Wanafunzi 16 Kiteto waliokatiza masomo kwa kupewa ujauzito warejeshwa shule

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Lt mstaafu John Henjewele akieleza namna bora ya kuwarejesha walio katishwa masomo kwa kupata ujauzito. Picha na Mohamed Hamad Kiteto
Muktasari:
- Jumla ya wanafunzi 16 waliokatishwa masomo yao kwa kupewa ujauzito wilayani Kiteto mkoani Manyara, sambamba na aina zingine za ukatili wamerejeshwa shuleni kuendelea na masomo yao
Kiteto. Jumla ya wanafunzi 16 waliokatishwa masomo yao kwa kupewa ujauzito wilayani Kiteto mkoani Manyara, sambamba na aina zingine za ukatili wamerejeshwa shuleni kuendelea na masomo yao.
Wakizungumza na Mwananchi digital leo Alhamisi Septemba 21, 2023 baadhi ya viongozi na wananchi wilayani Kiteto wamesema wengi wa wanafunzi wa kike wamekatishwa masomo kwa kupata ujauzito na hata umaskini wa wazazi wao kushindwa kuwaendeleza na kuiomba Serikali kuingilia kati kuendeleza ndoto zao
"Waliokatishwa masomo kwa kupata ujauzito huku vijijini wanapata shida kuwalea hao watoto wao waliowapata kwani hawawezi kwa sababu wamepata mimba wakiwa na umri mdogo," Shabani Sendalo mwenyekiti wa mtaa Kaloleni.
Wapo wazazi ambao watoto wao wamekatishwa masomo, wanapokuwa nyumbani wanakata tamaa ya kuishi na wanashindwa hata kuwasaidia hao watoto waliojifungua," amesema Jumanne Rashid Mohamed ambaye ni mwananchi Kiteto.
Akizungumzia lengo la awali la Serikali kwa mwanafunzi aliyepata mila, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kiteto, John Henjewele amesema lilikuwa kuonya wenye tabia hizo kuacha.
"Lengo la mwanzo kwa aliyepata mimba wakati ule na Serikali kuwaondoa shule ni asiambukize wasichana wengine udhaifu wake, ikaonekana ndani mwao wapo wanaopata mimba kwa ajali mbalimbali …wapo waliotumia mbinu wakaendelea na kusoma na leo ni viongozi wakubwa tu wanatoa mchango kwa jamii," Luteni mstaafu Henjewele.
Ili kurejesha ndoto za wanafunzi hao wa kike zilizokuwa zimeanza kupotea, Shirika la Kinnapa limekuja na mpango mkakati wa kuwarejesha shuleni wanafunzi hao kupitia Mradi wa Nipe Nafasi.
"Tutakaowasaidia ni wale waliokatisha masomo yao kwa kupata mimba za utotoni au changamoto ya ubakaji au kukosa mahitaji ya kujikimu shuleni mradi utamwezesha kumrudisha shuleni hadi atakapomaliza masomo yake," Paulina Ngurumwa ambaye ni mratibu Kitengo cha Maendeleo Shirika la Kinnapa.
"Jamii za Kimasai utamaduni na mila zinakandamiza mtoto wa kike haturuhusiwi kwenda shuleni tunaozeshwa umri mdogo na kunyimwa haki za msingi…Shirika la Kinnapa kupitia Mradi wa Malala Fund tunasaidia kupunguza madhara hayo kwa jamii," amesema Onike Yohana ambaye ni Laizer Mratibu Elimu Shirika la Kinnapa.
"Katika utekelezaji wa mradi huu tumeanzisha vilabu mashuleni kama sehemu ya watoto kujitetea kutoa taarifa za ukatili wanaofanyiwa nyumbani au shuleni na hata njiani walipokuwa wanaenda shuleni ama kutoka shule," Suzana Tuke wa Shirika la Kinnapa.
Afisa Ustawi wa Jamii Kiteto na waandishi wa habari waliozungumzima kuhusu mradi wa nipe nafasi, kurejesha ndoto za watoto wa kike na waliokatishwa masomo wanasema anasema jumla ya wanafunzi 16 wamerejeshwa shuleni.
"Sisi kama wilaya tuna kituo Kata ya Sunya ambako kuna watoto 16 wamesharudi na wanaendelea na masomo Serikali kadiri siku zinavyokwenda na wengine watajiunga na masomo yao," amesema Namshaki Mukare, Afisa Ustawi wa Jamii Kiteto.
"Mpango huu waliokuja nao Shirika la Kinnapa utasaidia sana jamii ya Kimasai, hii jamii iko nyuma haswa ubaguzi kwa mtoto wa kike elimu hii wenye fikra duni watoondokana nayo," Nyangusi Ole Sangida, mwandishi wa habari.