Wanafunzi 2,400 wasaidiwa taulo za kike

Muktasari:

  • Baadhi ya mila na tamaduni, suala la hedhi linapewa tafsiri potofu na hivyo kuongeza changamoto kwa watoto wa kike hali inayoathiri mahudhurio ya wanafunzi hao shuleni na wengi kujikuta wakiathirika kitaaluma.

Shinyanga. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), inakadiriwa msichana mmoja kati ya 10 kutoka nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara hukosa kwenda shule aingiapo kwenye mzunguko wake wa hedhi.

Hali hiyo imeelezewa kuwa ni miongoni mwa inayochangia watoto wengi wa kike katika nchi hizo kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu katika muda mwafaka.

Pia, imeelezwa kuwa baadhi ya mila na tamaduni, suala la hedhi linapewa tafsiri potofu na hivyo kuongeza changamoto kwa watoto wa kike hali inayoathiri mahudhurio ya wanafunzi hao shuleni na wengi kujikuta wakiathirika kitaaluma.

Hali hiyo pia inawakumba hata wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule nyingi nchini na miongoni ni wa mkoani Shinyanga.

Katika kuwanusuru na hali hiyo, Benki ya Benki ya Exim Tanzania imetoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi zaidi ya 2,400 wa Shule za Sekondari na Msingi zilizopo mkoani humo.

Shule hizo ni pamoja na ya Sekondari  ya Kiislamu Istiqaama,  Mwenge, Mapinduzi, Jomu, Ibadhi pamoja na  Kituo cha Agape aids control Programme zilizopo mkoani humo.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo jana, Meneja wa Benki hiyo tawi la Shinyanga, Sarah Paul alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa mpango wa uwajibikaji wa kwa jamii (CSR) wa benki hiyo unafahamika kama Exim Cares.

Alisema benki hiyo imekuja na mpango huo ili kusaidia wanafunzi wa kike kwa kuwapatia hitaji hilo muhimu kiafya sambamba na kutoa elimu kuhusu hedhi salama kwa wanafunzi pindi wakiwa shuleni.

Kwa mujibu wa Sarah, kupitia mpango huo, benki inatarajia kutoa misaada mingine kama hiyo kwa shule kadhaa katika mikoa mingine ikiwemo  ya Tabora na Iringa.

"Benki ya Exim imejitolea kikamilifu kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wanapata elimu, licha ya changamoto zinazowakabili na hili tutalifanikisha kwa kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kuwasaidia kuzitatua changamoto hizo na utoaji wa taulo hizi ni sehemu ya mkakati wa kukamilisha adhima hiyo,’’ alisema.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Istiqaama,  Mbaraka Songoro alisema msaada huo si tu unaonyesha utu, bali pia unaonyesha heshima kwa watoto wa kike.

"Sisi kama shule tunaona hii kama heshima kubwa kwa wapokeaji wa msaada huu na kwa jamii kwa ujumla. Misaada ya namna hii inaonesha namna watu na taasisi makini kama Benki ya Exim zinavyowachukulia watoto wa kike…tunashukuru sana ,” alisema.

Akitoa neno la shukrani kwa benki hiyo kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Fathihiya Faiz anayesoma kidato cha tatu Shule ya Sekondari Istiqaama, alisema mbali na uhitaji walio nao kwa bidhaa hiyo muhimu, pia wameupokea msaada huo kama ishara ya upendo na heshima kutoka kwa benki.

Na sasa itawafanya wasome wakitambua kuwa zipo taasisi na Watanzania wanaowajali na kutambua changamoto za kijinsia wanazopitia.

"Kwa msaada huu tunaamini hatutakabiliwa tena na magonjwa ambayo yanaweza kutokea kwa ukosefu wa taulo za hedhi. Pia msaada huu utaziba pengo ambalo wazazi wetu hawawezi kuliziba kwa sababu ya changamoto nyingi zinazowakabili zikiwemo za kiuchumi,’’ alisema.