Wanafunzi 48 kidato cha sita waliopata daraja la tatu muhula wa pili kutohamishwa shule za vipaji maalumu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania imesitisha uamuzi wa kuwahamisha wanafunzi 48 wa kidato cha sita waliopata daraja la tatu kwenye mitihani ya muhula wa pili katika shule za sekondari za vipaji maalumu kwenda shule za kawaida za bweni.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesitisha uamuzi wa kuwahamisha wanafunzi 48 wa kidato cha sita waliopata daraja la tatu kwenye mitihani ya muhula wa pili katika shule za sekondari za vipaji maalumu kwenda shule za kawaida za bweni.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Julai 19, 2019 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu mchakato huo uliotangazwa na Katibu wa wizara hiyo, Dorothy Gwajima.
Katika barua yake iliyokwenda kwa makatibu tawala wa mikoa iliyoandikwa Julai 12, 2019, Gwajima amesema Serikali inawahamisha wanafunzi kwenda shule za kawaida za bweni baada ya kupoteza sifa za kuendelea na masomo kwenye shule za vipaji maalumu.
Ofisi hiyo iliweka pia hadharani orodha ya majina 48 ya wanafunzi hao wanaosoma shule mbalimbali za vipaji maalumu za Kilakala, Msalato, Kibaha, Kisimiri, Ilboru, Mzumbe na Tabora Boys.
Hata hivyo, Jafo amesema Serikali imesitisha mchakato wa kuwahamisha wanafunzi hao na imeamuru kuendelee kubaki katika shule hizo kwa kuwekewa utaratibu maalumu utakaosaidia kukuza uwezo wao.
“Tumetafakari na nimeshamwagiza katibu mkuu (Gwajima), atoe maelekezo kuwa wanafunzi hawa wasihamishwe tena .Tutawaagiza walimu wa shule hizo kuongeza kasi na kuandaa programu maalumu itakayowajengea uwezo wa wanafunzi hawa,” amesema Jafo.
Jafo amesema uamuzi wa awali wa kuhamisha wanafunzi haukuwa na lengo baya bali walitaka kulinda hadhi ya shule hizo maalumu ili wanafunzi wanaosoma wawe na sifa zinazotakiwa.