Wanafunzi 900 Gairo wapatiwa taulo za kike
Morogoro. Wanafunzi 360 kati ya 900 wa kike sawa na asilimia 40 wa shule ya sekondari ya Gairo wilayani humo mkoani hapa wanashindwa kuhudhuria masomo kila mwezi wanapokuwa kwenye hedhi.
Muuguzi wa katika shule hiyo, Moshi Joseph amesema hayo wakati wa ugawaji wa taulo za kike za SoftCare zilizotolewa na kampuni ya DoweiCare inayofanya Kampeini ya kumfikia mtoto wa kike kielimu.
Amesema kuwa upatikanaji wa taulo hizo utaleta mwitikio wa wanafunzi kwa kasi kwani awali ilikuwa ikiwalazimu wasichana kurudi nyumbani kwa pindi anapopata hedhi akiwa shuleni ama wakati mwingine kushindwa kufika shule kwa siku tatu hadi nne na kumfanya kukosa masomo.
Mwanafunzi wa kidato cha tano, Grolia Wilson amesema zipo changamoto nyingi ambazo wasichana wasipokuwa na taulo wanazipata hasa wanapokuwa shuleni ikiwemo kukosa amani wakati wa kujisomea, kukosa masomo, kukaa nyumbani kwa muda mrefu na hiyo kupelekea kukosa vipindi vingi hivyo kurudisha nyuma maendeleo yao na kupelekea kutofaulu vyema.
“Nishukuru kwa huu msaada naamini sisi kama wanafunzi wa kike itatuongezea kuhudhuria masomo wakati wote tofauti na awali ilivyokuwa inatufanya tunakosa masomo kwa siku kadhaa na kukosa kujiamini wakati mwingine pindi unapoingia kwenye hedhi ukiwa shuleni,” amesema.
Kampuni hiyo ya DoweiCare licha ya kutoa taulo hizo kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 900 wa sekondari hiyo, pia wametoa msaada wa mahindi kilo 500 na maharage kilo 300 na kwamba matarajio ni kufikia shule tano (5) ambapo kwa sasa shule tatu za sekondari mkoa wa Morogoro zimefikiwa ambao ni Ngerengere, Morogoro Sekondari, na Gairo.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame akizungumza katika ugawaji huo wa taulo amesema wanafunzi wa kike katika maeneo mbalimbali nchini wana nafasi ya kufanya vizuri kitaaluma kutokana na serikali kuondoa vikwazo vingi na kutengeneza mazingira rafiki ya kujifunzia ikiwemo elimu bure, mikopo ya elimu ya juu,maabara kwa masomo ya sayannsi na mazingira rafiki ya kujistiri wakati wa hedhi.
“Hizi ni jitihada za serikali ambazo zimeendelea kufanyika hivyo maboresho ya maabara ya sayansi katika kila shule ili kuhakikisha mnasoma masomo ya sayansi kwa ajili ya maendeleo yenu na kwenye mazingira bora na rafiki ya kujisomea kwenu,” amesema Makame.