Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi kuandika matusi, Serikali na jamii yatwishwa zigo

Wanafunzi wakifanya mtihani. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Wanafunzi kuandika matusi kwenye mitihani ni changamoto ya maadili inayopaswa kufanyiwa kazi kwa haraka, wazazi watajwa kuchangia hali hiyo.

Dar es Salaam. Wakati  matokeo ya upimaji wa kitaifa kwa darasa la nne na kidato cha pili yakionesha wanafunzi 17 wakifutiwa matokeo kwa kuandika matusi kwenye mitihani yao, wito umetolewa kwa Serikali na jamii kwa ujumla kuwekeza katika kuwafundisha watoto umuhimu wa elimu.

Taarifa ya matokeo hayo yaliyotangazwa leo Jumapili, Januari 7, 2024 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Said Mohamed imeonesha wanafunzi watatu wa darasa la nne na 14 wa kidato cha pili waliandika matusi kwenye karatasi zao.

Dk Mohamed amesema suala hilo ni la kimaadili na wataziwasilisha karatasi hizo kwa wakuu wa shule husika ili hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wanafunzi waliofanya kitendo hicho.

Hii si mara ya kwanza kwa Necta kufuta matokeo ya wanafunzi walioandika matusi kwenye karatasi zao za mitihani.

Matukio ya aina hiyo yalitokea mwaka 2019 ambapo wanafunzi wawili wa kidato cha nne walifutiwa matokeo kwa kuandika matusi katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2018.

Pia, iliwafutia wanafunzi 14 walioandika matusi katika upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili mwaka 2022.

Mbali na matusi miaka ya nyuma imeshawi kuripotiwa matukio ya watoto kuchora vibonzo na kuandika nyimbo za bongofleva kwenye karatasi za mitihani.

Tabia hii ambayo imeanza kuwa sugu imepokelewa kwa mitazamo tofauti na wadau wakihoji sababu zipi zinazowafanya watoto wafikirie na kuandika matusi kwenye mitihani.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Maadili Centre, Frolentine Senya amesema vitendo hivi vikiendelea kuvumiliwa suala la mmomonyoko wa maadili litaendelea kutikisa vizazi hadi vizazi.

Senya amesema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye miundombinu ya elimu bado watoto hawapati fursa ya kufundishwa au kuona umuhimu wa elimu hivyo wanajikuta wakifanya mambo yasiyofaa kwenye mitihani ili na wao waingie kwenye mfumo mbovu wa maisha unaowazunguka.

Mtaalam huyu wa malezi anaelekeza pia lawama kwa wazazi kwa kukosa muda wa kuzungumza na watoto wao na kuwaeleza umuhimu wa elimu na matunda ambayo mtu anayapata akisoma.

“Watoto hawafundishwi umuhimu wa elimu tofauti na ilivyokuwa zamani mtoto anatamanishwa kuwa daktari, mwalimu, mwanasheria na fani nyingine nyingi.

Wanayoyaona kwa waliowatangulia hayawapi taswira njema ya kuichangamkia elimu. Hawapati fursa ya kuwaona waliosoma na kufanikiwa matokeo yake wanatumia muda mwingi kuwaangalia waliopitia njia za mkato kufanikiwa,” amesema Senya na kuongeza:

“Akikaa huku anaona wasanii, akigeuka kule anawaona watu maarufu mitandaoni na jinsi wanavyofanikiwa na ukweli ni kwamba hao sio mfano mzuri hivyo haoni umuhimu wa elimu na ndiyo maana si shida kwake kuandika matusi kwenye karatasi ya mtihani.”

Kwa upande wake, Mwalimu Bahati Hyera amesema jamii haitakiwi kuvumilia utovu huo wa nidhamu unaofanywa na watoto kwa kuwa ndiyo chanzo cha kutengeneza kizazi cha watu wasio na maadili.

“Tunaona watu wanashinda mitandaoni wakitukana watu, sasa tukiwaacha hawa watoto wakue katika msingi huu ni wazi tunatengeneza kizazi cha hovyo, mzazi ni lazima uwe karibu na mtoto wako, umfundishe yaliyo mema, kuna sehemu tunakosea kwenye malezi huu mzigo wasiangushiwe walimu,” amesema Bahati.

Licha ya kukiri kuna changamoto kwenye malezi, Jane Nzige ambaye ni mzazi amesema utandawazi unachangia kwa kiasi kikubwa watoto kujifunza vitu visivyofaa na matokeo yake wanaviandika kwenye mitihani.

“Ukweli ni kwamba utandawazi umefanya watoto wajifunze na wayaone mengi, sasa inapotokea hana cha kujibu kwenye mtihani anaona bora aandike vitu vya hovyo, ushauri wangu nguvu kubwa itumike katika kuwajenga kwenye misingi mizuri wajue kwanini wanasoma na wafundishwe kuwa raia wema,” amesema Jane.