Wanafunzi Veta waililia Serikali mikopo

Muktasari:
Chuo cha Veta Kagera kilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mwaka 2022 na kina uwezo wa kudahili wanafunzi 400 wa kozi ndefu na wengine 1, 000 kozi fupi kwa mwaka.
Bukoba. Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na Huduma Mkoa wa Kagera wameomba Serikali kutoa mikopo kwa kada hiyo kuwezesha watoto wanaotoka familia zisizo na uwezo kifedha kujiunga na mafunzo hayo.
Wakitoa maoni yao mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, wanafunzi hao wamesema kukosa mikopo siyo tu kunapunguza idadi ya wanaojiunga vyuo vya ufundi, bali pia huathiri mafunzo kwa vitendo nje ya chuo kwa wengi wao kutomudu gharama.
Aderitus Bruno, mwanafunzi wa kozi ya umeme chuoni hapo amesema Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati kutawezesha Taifa kuwa na wataalam wengi wenye ujuzi wa kati watakaosaidia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
"Kama inavyotoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali ifanye hivyo pia kwa sisi wa vyuo vya kati ili kutuwezesha kukabiliana na tatizo la kiuchumi linalotukwamisha kufikia malengo yetu kielimu,’amesema Bruno
Hoja hiyo imeungwa mkono na Diana Michael, mwanafunzi wa kozi ya umeme wa nyumbani akisema baadhi ya wanafunzi wa vyuo vya ufundi kutoka familia zenye uwezo mdogo kiuchumi hukumbana vikwazo kadhaa ikiwemo kusogeza mbele kwa muda au kukatisha masomo.
"Wazazi wetu hawalingani kimapato, wapo wanaomudu kulipia gharama zote za masomo kwa watoto wao na wengine wanalipia kwa awamu….tunaiomba Serikali itusaidie kwa kutupatia mikopo,’’ amesema Diana
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Omar Kipanka amesema suala la mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati tayari limejadiliwa na kupitishwa bungeni na kilichosalia ni utekelezaji.