Waziri Mkenda ataja sifa za wahitimu kupata Samia Scholarship

Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wanafunzi wanufaika wa Samia Scholarship
Muktasari:
- Serikali imetenga kiasi cha Sh6.7 bilioni kwa ajili kwa ajili ya dirisha la ufadhili (Samia Scholarship) kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya kidato cha sita.
Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imetenga Sh6.7 bilioni kwa ajili ya ufadhili (Samia scholarship) ambapo wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita, watanufaika.
Profesa Mkenda amesema ufadhili huo utahusisha ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, posho ya vitabu, mahitaji maalum ya vitivo, vifaa saidizi kwa wenye mahitaji maalum na bima ya afya.
Mkenda ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 27, 2023 wakati akitangaza ufadhili huo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema ufadhili huo wa asilimia 100 ulianza mwaka 2022 kwa kuwachukua wanafunzi 636 wakiwemo wasichana 261 sawa na asilimia 41 na wavulana 375 kwa asilimia 59 pamoja na wanafunzi 12 wenye mahitaji maalum ambapo kiasi cha Sh3 bilioni zilitumika.
"Kwa mwaka wa fedha 2023/24 tunatarajia kuchukua wanafunzi 640 waliohitimu kidato cha sita na Sh6.7 bilioni zimetengwa kwa wanafunzi wa zamani wanaoendelea na hawa wapya," amesema Profesa Mkenda.
Amesema ingizo jipya litafanya jumla ya wanafunzi 1,276 na ufadhili huu ni kwa masomo ya shahada ya kwanza waliofaulu mwaka 2023.
"Lazima uwe umefanya mtihani wa baraza la mitihani na umefanya vizuri kwenye masomo ya sayansi, umefaulu zaidi kuliko wenzako na ufadhili huu utaendelea kutokea GPA ya 3.8 ukishuka tutakuondoa kwenye ufadhili wa Samia Scholarship na utarudi kwenye mikopo," amesisitiza Profesa Mkenda.