Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi bonde la Msimbazi wampinga Waziri Mabula

Mwenyekiti wa Kamati ya Walalamikaji Mradi wa bonde la Msimbazi Charles Swai akizungumza katika mkutano na wananchi.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula kutamka bungeni kuwa wakazi wanaoishi kando ya bonde la Msimbazi wamekubali kuhakikiwa, wananchi hao wameibuka na kumpinga waziri huyo.

Aprili 13, 2023 bungeni mjini Dodoma  Mabula alisema asilimia 92 ya wananchi hao wameridhia kuhakikiwa.

Jana Jumamosi Aprili 14, 2023 katika mkutano wa wananchi uliofanyika eneo la Kigogo, mwenyekiti wa kamati ya walalamikaji mradi wa bonde la Msimbazi, Charles Swai kwa niaba ya wananchi hao amesema wanapinga kauli hiyo ilitolewa na Mabula bungeni.

"Sio kweli kwamba asilimia 92 wamekubaliana na uhakiki hasa kiwango ambacho kimetolewa kutulipa. Hakuna mbunge aliyekaa na wananchi na hata hatujui habari hizi waziri kazipata wapi, kwa sababu watu waliolipwa hela wamelipwa kiwango tofauti kabisa na thamani ya nyumba zao," amesema Swai.

Swai amesema wananchi hao hawakubaliani na tathmini iliyofanyika, na kwamba  waziri huyo alizungumzia  ambao walikataa kabisa kusaini kupokea fedha ndio ambao watafanyiwa uhakiki na sio ambao wamelipwa kiwango kidogo.

Hamisi Juma amesema kwa kuwa mradi huo unafadhiliwa  na  Benki ya Dunia, ikiwezekana wazungumze na mwakilishi wa benki hiyo moja kwa moja.

"Tukae na mtu wa benki ya Dunia tumpatie malalamiko yetu ili ayapeleke ofisini kwao tuone kama ataweza kutusaidia. Tumfanye mtu wa benki ya Dunia kama mtetezi wetu, maana sisi hatuna mtetezi," amesema Juma.

Mjumbe wa mtaa wa Madaba Bondeni,  Jamila Juma amesema alimuomba mwenyekiti wa kamati ya walalamikaji mradi wa bonde la Msimbazi kufanya utaratibu wa kukutana na mbunge kupokea malalamiko ya wananchi wake lakini kabla ya kukutana na mbunge ndipo aliposikia taarifa bungeni kwamba asilimia 92 wameridhia kiwango walicholipwa jambo ambalo sio kweli.

"Tunamuomba waziri afute kauli yake hiyo maana si kweli, kila mtu analalamika, hakuna hata mmoja aliyekubali kiasi hicho," amesema Jamila.

Jamila amemuomba  Mabula kufuatilia kwa wananchi wenyewe na kujua ukweli  badala ya kuamini alichoelezwa.

Jamila amesema walitia saini kupokea viwango hivyo ambavyo havina thamani sawa na nyumba sio kwa hiyari bali kwa kulazimishwa huku wakitishiwa kwamba kama wasingesaini fedha zingepelekwa katika huduma za kijamii.

"Nilisaini na niliandika barua ya malalamiko kama ambavyo tulielekezwa, lakini baada ya kupeleka barua siku kadhaa mbele, ilikataliwa nikiambiwa   nilitakiwa kuandika siku ambayo nilisaini hela jambo ambalo hawakulisema siku tukiwa tunasaini, ni kama kuna ujanja tunafanyiwa. Tumepigwa, " amesema Jamila.

Katika maelezo yake bungeni, Mabula amesema wananchi 2217 kati ya 2432 sawa na asilimia 92 wamehakikiwa na wamekubali huku 160 wakiwa bado ila watakapofikiwa watapata huduma sawa na waliyopatiwa wenzao.