Wananchi Busega waomba msaada wa chakula

Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Yahya Nawanda wilayani Busega uliolenga kusikiliza kero za wananchi. Picha na Samirah Yusuph

Muktasari:

  • Wananchi hao wamesema njaa imeathiri na kushusha shughuli za uzalishaji hali inayochangia kuchelewesha shughuli za maendeleo ikiwamo kuwapeleka watoto

Busega. Kutokana na hali ya ukame iliyosababisha njaa katika baadhi ya maeneo nchini, wananchi wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu wameiomba serikali kuwaletea chakula kitakachouzwa bei nafuu ili kuwanusuru na janga la njaa.

Ombi hilo limetolewa leo Januari 24, 2023 katika siku ya pili ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Yahya Nawanda wilayani Busega ambapo baadhi ya wananchi walieleza kuwa hali ya ukame imeathiri uzalishaji na kusababisha vyakula kupanda bei.

"Vifaa vya shule vipo juu, bei ya vyakula ipo juu tofauti na kipato cha mtu, tunaomba watuletee chakula wa sababu nchi yetu imekabiliwa na ukame hivyo tukipata chakula cha bei nafuu itasaidia kupunguza njaa katika familia zetu," amesema Leah Wilson mkazi wa Nyamikoma.

Naye Peter Makelemo mkazi wa Nyamikoma amesema, kutonyesha mvua kwa muda mrefu ndio kumesababisha njaa kali.

“Njaa ni kali chakula kinapatikana kwa garama kubwa," amesema.

Kwa sasa wilaya hiyo inategemea mahindi kutoka mikoa ya Katavi na Rukwa ambayo yanauzwa Sh21,000 hadi Sh27,000 kwa ndoo ya lita 20huku mchele ukiuzwa Sh25,00 hadi Sh35,000.

Kwa upande wa mkuu wa Mkoa wa Simiyu Yahya Nawanda akijibu kuhusu janga hilo amesema serikali kupitia mfuko wa chakula nchini umejipanga kuleta chakula kwenye maeneo ambayo yanakabilowa na njaa.

Amesema chakula hicho kitauzwa kwa bei nafuu ili kila mwananchi amudu gharama za kununua hali itakayo punguza kwa kiasi kikubwa njaa iliyopo na kuwasogeza katika msimu wa mavuno.

"Mahindi yataletwa kwenye maeneo yenye njaa na watakuwa wanauza wenyewe pia wakija muwaelekeze katika vijiji vingine ili waende kupeleka vyakula huko, njaa haipo hapa pekee," amesema nawanda

Kwa msimu wa kilimo 2021/22 tani 588,911 za mazao ya nafaka zilizalishwa mkoani Simiyu ikilinganishwa na tani 500,000 zilizotarajiwa.