Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi Kingolwira wanavyotaabika kusaka huduma za kujifungua kwa upasuaji

Jengo la mapokezi kwa wagonjwa wa nje katika kituo cha afya Kingolwira kilichopo Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff



Muktasari:

  • Kutokana na kukosekana kwa huduma ya upasuaji, wajawazito 60 hadi 70 kwa mwezi wanapewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Morogoro. Takriban wajawazito 60 hadi 70 katika eneo la Kingolwira mkoani Morogoro, wanalazimika kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kupata huduma ya kujifungua kwa njia ya upasuaji kila mwezi.

Hatua hiyo inatokana na Kituo cha afya Kingolwira, kilichopo karibu nao, kukosa huduma hizo, hali inayowapa wananchi tabu kufuata huduma mbali na maeneo wanayoishi.

Hayo yameelezwa leo Jumapili, Julai 5, 2026 na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha Kingolwira, Dk Charles Sabini, alipotoa taarifa ya kituo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kingolwira, Dk Charles Sabini (kushoto, mwenye koti jeupe), akitoa maelezo kuhusu utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Paramagamba Kabudi (kulia, mwenye miwani), alipotembelea kituo hicho katika Manispaa ya Morogoro kukagua hali ya huduma kwa wananchi. Picha na Hamida Shariff.

Amesema idadi hiyo ya wajawazito wanaopewa rufaa ni kwa mwezi mmoja, hatua inayosababisha msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo ya rufaa.

Mbali na kukosekana kwa huduma hiyo, Dk Sabini amesema changamoto nyingine inayowakabili ni kukosekana kwa mashine ya X-ray.

Amesema hawana mashine hiyo, huku kituo hicho kikipokea majeruhi wengi wa ajali, hali inayowalazimu kuishia kutoa huduma ya kwanza na kuwapa rufaa wagonjwa.

“Kituo chetu kipo kando ya barabara na mara nyingi tumekuwa tukipokea majeruhi wa ajali waliopata mivunjiko. Hatuwezi kutoa matibabu kwa sababu hatuna mashine ya X-ray,” amesema.

Jengo la maabara la Kituo cha afya Kingolwira kilichopo Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff

Caren Mkama, mkazi wa Kingolwira, amesema huduma ya upasuaji ni muhimu katika kituo hicho kinachopokea wajawazito kutoka vijiji vya jirani kama Mikese, Mkambarani, Pangawe, Newland na Mtego wa Simba.

“Unaweza ukamleta mjamzito hapa, baada ya kupimwa akaonekana hawezi kujifungua kawaida, inabidi apewe rufaa kwenda hospitali ya mkoa. Kule mjini huna ndugu wala jamaa, hivyo unajikuta unatumia gharama kubwa,” amesema.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Profesa Kabudi amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya na kuhakikisha vituo vya afya vinajengewa uwezo wa kutoa huduma bora ili kupunguza msongamano kwenye hospitali za wilaya na za rufaa.

Ametaja moja ya maeneo yanayoboreshwa kuwa ni upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na wataalamu wa kutosha.

Katika ziara hiyo, Profesa Kabudi pia amekagua mashine za kisasa za kutolea kondomu na vifaa vya kupimia maambukizi ya virusi vya Ukimwi, zilizonunuliwa na kufungwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha Mzumbe.