Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wajenga zahanati yao kijiji kilichokosa huduma tangu 1976

Mwenyekiti wa umoja wa vijana katika kijiji cha Irienyi wilayani Rorya, Fredrick Kichere akiwa na beseni wakati wa harambee kwaajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Umoja wa Vijana wa Kijiji cha Irienyi, Kata ya Komuge wilayani Rorya Mkoa wa Mara umechanga zaidi ya Sh27 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho mradi uliokwama kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Rorya. Umoja wa Vijana wa Kijiji cha Irienyi, Kata ya Komuge wilayani Rorya Mkoa wa Mara umechanga zaidi ya Sh27 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho mradi uliokwama kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Fedha hizo tayari zimetumika kujenga boma la zahanati hiyo huku umoja huo ukiiomba serikali kuwasaidia ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo mradi ambao unatarajiwa kugharimu Sh200 milioni hadi kukamilika.

Mwenyekiti wa umoja huo, Fredrick Kichere amesema leo Septemba 15, 2022 kijijini hapo kwenye harambee iliyoitishwa na vijana hao kwa lengo la kupata fedha kwaajili kupaua jengo hilo, amesema waliamua kujenga zahanati hiyo kutokana na ukosefu wa kituo cha kutolea huduma kijijini hapo.

" Tangu tumezaliwa tumekuwa tukishuhudia wazazi wetu jinsi wanavyopata shida wakati wakitafuta huduma ya afya, tumeshuhudia vifo vya watoto wachanga pamoja na akinamama wanaotaka kujifungua kutokana na kutokuwa  na huduma ya afya karibu tukaamua kuwa lazima vijana wa kijiji hiki tufanye jambo" amesema.

Amesema kuwa mwaka jana  kwa pamoja vijana hao walikubaliana kuchangia Sh5,000 kila mwezi na ilipofika mwezi Septemba mwaka huo wakaanza ujenzi wa jengo hilo chini ya usimamizi wa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Rorya ambapo hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa boma  pamoja na kuweka madirisha na milango.

Diwani wa Kata ya Komuge, William Marwa amewapongeza vijana hao na kusema kuwa zahanati hiyo itasaidia wakazi wa kijiji hicho pamoja na kata nzima kutokana kata hiyo kutokuwa na kituo cha afya hali ambayo imekuwa ikipelekea wakazi wake kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya

"Hii kata ina vijiji vinne lakini hakina kituo cha afya kwa hiyo wakazi wake wanalazimika kwenda Kinesi au Kowaki  kwaajili ya  huduma ya afya niiombe serikali itusaidie kuweka miundombinu ya kutosha ili hii zahanati iwe kituo cha afya kabisa," amesema.

Mgeni rasmi katika harambee hiyo, ambaye ni mfanyabiashara wa jijini Mwanza, Majani Masagati amewataka wazaliwa wa kijiji hicho wanaoishi nje ya mkoa kuwaunga mkono vijana hao ili waweze kutimiza dhamira yao.

" Niwaombe vijana wenzangu wazaliwa wa kijiji hiki na kata hii mlioko nje ya eneo hili, njooni tuwaunge mkono vijana wenzetu kwa wazo lao hili zuri. Mkumbuke kuwa hakuna mtu wa kukuletea maendeleo isipokuwa ni sisi wenyewe na hata tukitaka serikali ituunge mkono lazima tuanze kwanza sisi," amesema.

Mtendaji wa Kata ya Komuge, James Shadrack amesema kuwa wakazi wa kijiji hicho wanalazimika kutembea zaidi ya komita 16 na 25 kwenda kutafuta huduma ya afya katika kituo cha afya Kinesi au Hospitali ya Kowaki kutokana na kijiji hicho kutokuwa na sehemu ya kutolea huduma ya afya.

" Pamoja na kuwa kata hii ina wakazi zaidi ya 16,000 na kijiji hiki pekee kikiwa na watu zaidi ya 6,000 lakini hakuna sehemu ya kupata huduma ya afya hivyo wanalazimika kutembea zaidi ya komita 16 hadi 25 kwenda Kinesi na Kowaki kwa hiyo hii zahanati itakapokamilika itakuwa mkombozi sio kwa Irienyi pekee bali kwa vijiji vyote vinne vya kata ya Komuge," amesema.