Wananchi wasota siku 21 bila kivuko

Boti zinazotumiwa na wakazi wa Kata ya Kitumbikwera Manispaa ya Lindi baada ya Kivuko cha Mv Kilambo kuharibika kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa upoozaji. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Wananchi wanaoishi katika maeneo ya Kitunda katika Kata ya Kitumbikwera, Manispaa ya Lindi, wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na kivuko kwa zaidi ya siku 21
Lindi. Wakazi wa Kata ya Kitumbikwera katika manispaa ya Lindi, wameiomba Serikali kuharakisha matengenezo ya kivuko kilichopo katika eneo lao ili waendelee na shughuli za uzalishaji mali.
Kuharibika kwa kivuko cha MV Kitunda, kumesababisha wananchi hao kutumia boti zinazodaiwa si salama zenye kuhatarisha maisha yao.
Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo Alhamisi Novemba 16, 2023, wananchi hao wamesema Serikali isipoharakisha matengenezo wataathirika zaidi kiuchumi.
Dadi Fikiri ni mkazi wa kata hiyo, amesema walishazoea kutumia njia ya maji kwa kuwa ni rahisi tofauti ile ya barabara yenye urefu wa zaidi ya kilometa 75 hivyo ni vema Serikali ikawapelekea kivuko kingine kwa kuwa boti wanayotumia haikidhi mahitaji yao.
"Baada ya kuharibika kivuko cha MV Kitunda, tukaletewa kivuko kingine cha MV Kilambo ambacho nacho kimeharibika, sasa hivi tunapata shida, kwa hiyo kuna boti za uvuvi ndiyo tunatumia, moja ikienda nyingine inarudi ili watu wasisubiri kwa muda mrefu," amesema Dadi
Dadi amesema: “Wanafunzi na wanawake wajawazito wanapata shida sana, kama watoto wanatakiwa waende shuleni kila siku, usafiri wenyewe ni wa hatari, boti kama hii ya kuvulia samaki ni ndogo wanaingia watu na mizigo ni hatari sana.” amesema
Baadhi ya wanawake ambao hawakutaka kutaja majina yao wamesema kuwa changomoto wanayoipata ni kubwa hivyo wanaiomba Serikali kuwaletea kivuko kingine.
“Tunashindwa kutaja majina yetu kwasababu unapojitambulisha wamekuona tu sehemu, hawa wanaofanya kazi kwenye kivuko wanatufuata na kuanza kukusemea maneno mabaya,” amesema mmoja wa wanawake hao.
Mkazi wa Nampunga, Juma Selemani amesema kuwa kivuko kinaharibika mara kwa mara, Serikali ijitahidi kuleta kivuko kingine kilicho bora zaidi, kwa kuwa wengi wa wananchi wanaotoka Kitumbikwera, hufanya shughuli za kiuchumi wanafanyia mjini.
“Tunaomba tuboreshewe kivuko...mahitaji yote tunayapata mjini kwa hiyo lazima tuje kufuata mahitaji yetu huku wengine wakija kwenye shughuli zao,” amesema Juma.
Kwa upande wake Fortunatus Mruke ambaye ni msimamizi wa kivuko cha MV Kilambo, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuahidi kulifanyia kazi kwa haraka.
Kweli kuna changamoto ya kuharibika kwa kivuko, kumetokea itilafu kwenye mfumo wa upoozaji, niwaombe wananchi kuwa wavumilivu kwenye kipindi hiki,” amesema Mruke.