Wanaodaiwa kusafirisha wenye ulemavu, kuwatumia kuomba wafikishwa mahakamani

Wednesday January 13 2021
New Content Item (1)
By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Watu 15 akiwemo mfanyabiashara, Sadikiely Meta (71) wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu kinyume cha sheria, kukwepa kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh31 milioni.

Meta na wenzake wanadaiwa kusafirisha wenye ulemavu 37, wakiwemo watoto wadogo wenye umri wa miaka saba na 11 kutoka mikoa ya Tabora, Shinyanga na kuwaleta Dar es Salaam na kisha kuwataka waombe fedha mitaani ili wao wajiingizie kipato.

Mbali na Meta washtakiwa wengine ni

Yusuph Mbuani, Joseph Magafu, Emmanuel Salu, Gogad Mayenga, Samson Akunahai, Husein John  na wenzao nane.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Jumatano Januari 13, 2021 na wakili wa Serikali mwandamizi, Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon mbele ya hakimu mkazi mkuu, Kassian Matembele.


Advertisement

Wakili Mshanga amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2021.

Katika shtaka la kwanza, Meta na wenzake wanadaiwa kati ya Agosti 2020 na Januari mosi 2021 jijini Dar es Salaam wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu uliosababisha biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Shtaka la pili, ambalo ni kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Agosti 2020 na Januari mosi, 2021 katika eneo la Tandale wilaya ya kinondoni walisafirisha watu wenye ulemavu 37 wakiwemo watoto wadogo wenye umri wa miaka saba na 11.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwasafirisha walemavu hao kutoka mikoa ya Shinyanga na Tabora  na kuwaleta Dar es Salaam na kisha kuwatumikisha katika shughuli ya kuomba barabarani kwa lengo la kujipatia fedha na kwamba kwa kitendo hicho washtakiwa hao walijinufaisha kwa kupata fedha zilizotokana na biashara hiyo ya usafirishaji.

Wakili Simon amedai katika shtaka la kukwepa kodi linalomkabili Meta peke yake, inadaiwa kati ya Agosti 2018 na Januari mosi, 2021 Dar es Salaam, mshtakiwa alishindwa kulipa kodi kwa TRA ya Sh31,328,015.

Pia, Meta anadaiwa kuisababishia TRA hasara ya kiasi hicho pamoja na kutakatisha fedha hizo.

Wakili Simon amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Matembele baada ya kusikiliza kesi hiyo amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa makosa ya kusafirisha binadamu hayana dhamana.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, 2021 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Advertisement