Wanaoutaka uspika wafika 17

Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solom Itunda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Muktasari:

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania wamefika 17 baada ya wengine nane kuchukua leo Jumanne Januari 2022.

Dodoma. Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania wamefika 17 baada ya wengine nane kuchukua leo Jumanne Januari 2022.

Wanachama hao nane wamejitokeza kuendelea kuchukua fomu hizo katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma na wengine kwenye ofisi ndogo Lumumba jijini Dar es Salaam.

Idadi hiyo ya waliochukua fomu leo inafanya jumla ya wanachama wa chama hicho kuwa 17 ambapo tisa walichukua jana Jumatatu siku ambayo ratiba hiyo ilianza.

Akitoa taarifa ya mchakato huo wa uchukuaji fomu leo Katibu Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa, Solomon Itunda amesema kwa upande wa Dodoma wamejitokeza wanachama watatu ambao ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, Emmanuel Mwakasaka na Profesa Henry Mpoki.

Amesema kwa upande wa ofisi ndogo ya chama hicho Dar es Salaam wamechukua watano akiwamo Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku 'Msukuma', aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba na akiyewahi kuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye,  Juma Hamza na Baraka Byabato.

Itunda amesema licha ya kesho kuwa sikukuu ya maadhimisho ya Mapinduzi Zanzibar ofisi zitakuwa wazi kwa ajili ya kuwapa nafasi wanachama kuchukua na kurudisha fomu huku akisema kwa upande wa ofisi za Zanzibar hakuna mwanachama aliyejitokeza kuchukua fomu.

“Kwakuwa zoezi limeanza tarehe 10 na mpaka tarehe 15 tupo na tumebakisha siku zaidi mbele, kwahiyo ni matumaini yangu watajitokeza wanachama wa chama cha Mapinduzi Zanzibar kwakuwa ni suala la muda tu” amesema