Wanawake kujengewa uwezo masomo ya sayansi
Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Kamal Okba, na Mwakilishi wa UN Women Tanzania, Hodan Addou wakionyesha nyaraka za makubaliano (MoU) waliyosaini leo kwa lengo la kuwawezesha na kuwajengea uwezo wanawake na wasichana wa Kitanzania katika eneo la STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati) pamoja na stadi za uandishi wa dijitali.
Muktasari:
- Shirika la UN Women kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano Tigo, wamesaini makubaliano ya kusaidia wasichana na wanawake wa vijijini na mijini kujifunza masomo ya sayansi.
Dar es Salaam. Katika kuiongezea nguvu programu ya 'Code like a Girl' inayohamasisha kujifunza masomo ya sayansi (STEM), UN Women Tanzania limesaini makubaliano na Tigo Tanzania ili kuongeza ujuzi wa kidijitali miongoni mwa wanawake na wasichana mijini na vijijini.
Programu hiyo itakayohusisha ujifunzaji katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati na stadi za uandishi wa kidijitali, imelenga kutoa mafunzo hayo kwa wanawake na wasichana wenye umri wa miaka 17 hadi 25 ili waweze kusoma taaluma hiyo.
Takwimu za tafiti mbalimbali zinaonyesha takribani asilimia 90 ya kazi zijazo duniani zitahitaji ujuzi wa Tehama.
Hata hivyo uandikishaji katika masomo ya sayansi unaonyesha pengo kubwa la kijinsia ambapo wasichana wachache kuliko wavulana.
Akizungumza leo Jumanne, Novemba 21, 2023 katika hafla ya kutiliana saini, Mwakilishi wa UN Women Tanzania, Hodan Addou amesisitiza umuhimu wa kuwajumuisha wasichana katika sekta ya Tehama kama jambo la lazima, ili kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nyanja hizo.
“Wanawake wanaposhiriki katika Tehama, huleta mitazamo tofauti ambayo ni muhimu kwa uvumbuzi na matokeo bora.
“Ushirikiano huu na Tigo sio tu kuhusu kuweka usawa bali kuandaa mazingira ambayo wanawake wana fursa sawa za kujifunza, kufaulu na kuongoza,” amesema.
Amesema, “Kushirikisha sekta kibinafsi ni muhimu katika kupanua fursa na kutoa mifano inayoonekana kwa wasichana wanaotaka kufanya kazi za teknolojia.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Kamal Okba amefurahishwa na ushirikiano huo akisema, "Katika ulimwengu unaoendeshwa na uvumbuzi na muunganiko wa kidijitali ni muhimu tusimwache mtu nyuma.
Amesema kupitia mradi wa Binti Digitali, wamedhamiria kuziba pengo la jinsia katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ambapo Tigo itajitolea kutoa mafunzo hayo pamoja na mchango wa muunganisho wa intaneti wa kasi ya juu wa 4G na 5G.
Kamal amesema ni ngumu kusema kwamba watawafikia wangapi kwa sababu uhitaji ni mkubwa na jambo hilo litafanyika kwa nchi nzima.
"Ushirikiano huu unaashiria hatua kubwa kuelekea kuongeza ujuzi kwa kundi hili, pia kuchangia kupunguza pengo katika ajenda pana ya uchumi wa kidijitali. Kwa pamoja tunaweza kuleta mafanikio chanya katika sekta ya mawasiliano,” amesema Kamal.