Wanawake waelezwa jinsi ya kujikwamua kiuchumi

Muktasari:

Ujasiri na uthubutu  ni silaha ambazo mwanamke anapaswa kuwa nazo ili kujiandaa kuwa mama bora na  kuikomboa jamii kiuchumi.

Dar es Salaam. Ujasiri na uthubutu  ni silaha ambazo mwanamke anapaswa kuwa nazo ili kujiandaa kuwa mama bora na  kuikomboa jamii kiuchumi.


Kauli hiyo ilitolewa leo Alhamisi Machi 4, 2021 kwenye semina ya wanawake iliyoandaliwa na Gloria Anderson, mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya (TEDI) inayoshughulika na masuala ya utoaji  elimu ya ubunifu kwa wanawake.


Ameshauri kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani  Machi 8, 2021 ambayo kitaifa yatafanyika jijini Dodoma, mwanamke yeyote anapaswa kujitambua kwa kutumia vyema fursa  anayopata kwa kufanya kazi  kwa weledi sehemu yeyote kwa ajili ya kujitengenezea kesho yake.


"Watu wajitahidi kufanya kazi kwa ujasiri na kujituma kwa kuonesha ubunifu wa kipekee,  wasiogope kujifunza au kutoa gharama kwakuwa kupitia shughuli hizo wanatengeneza mahusiano mazuri ya kujitegemea.”


"Kikubwa wanawake tunapaswa kuwa na uthubutu na ujasiri na usifanye kazi kwa kuwa watu wanafanya,  fanya kitu unachokipenda itakuwa rahisi kukabiliana na changamoto zitakazokukuta na mwisho wa siku utafanikiwa kiuchumi na kuikomboa jamii," amesema Gloria


Mmoja wa washiriki, Mary Mweleka amesema wanawake wasichague kazi na wala  wasiogope kufanya kazi bure.


“Unajua kujifunza vitu tofauti havikufanyi kupoteza malengo uliyojiwekea bali unajifunza kwa faida ya baadaye ili utakapokuja kuanzisha kampuni yako unakuwa umeshazoea na unakuwa na wigo mkubwa  kwa mambo mengi," amesema Mary.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda