Wanyama waharibifu wazidi kuwatesa wananchi

Mbunge wa Moshi Vijiji (CCM) Profesa Patrick Alois Ndakidemi akiuliza swali katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali yatoa wito kwa wananchi Kilimanjaro kutoa taarifa mara wanaposumbuliwa ama kuvamiwa na wanyama waharibifu kwakuwa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ina vituo vya askari wanyamapori kwenye wilaya inazopana nayo.

Dodoma. Serikali yatoa wito kwa wananchi Kilimanjaro kutoa taarifa mara wanaposumbuliwa ama kuvamiwa na wanyama waharibifu kwakuwa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ina vituo vya askari wanyamapori kwenye wilaya inazopana nayo.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Khamis, alipokuwa akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

Khamisi amevitaja vituo hivyo ni Hifadhi (Moshi - vituo 4, Rombo - vituo 3, Hai - kituo 1, Siha - kituo 1 na Longido - vituo 2) na kwamba vituo hivyo vina askari wa Jeshi la Uhifadhi ambao kwa kushirikiana na maafisa wa wanyamapori kutoka Wilaya husika wamekuwa wakifanya kazi ya kuwafukuza wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi ya Wananchi au mashamba yao.

Naibu Waziri huyo mesema ni muhimu kutoa taarifa kwa Askari wa Uhifadhi wa vituo hivyo pale wanyamapori hao wakiwemo nyani, kima, tumbili na ngedere, wanaingia kwenye maeneo yao ili waweze kudhibitiwa na kuzuia madhara.

Awali, Mbunge wa Moshi Vijiji Profesa Patrick Alois Ndakidemi (CCM) aliomba kujua Serikali ina mpango gani wa kutatua kero ya nyani, kima, tumbili na ngedere kwa Wananchi wanaopakana na Mlima Kilimanjaro.

Mbunge huyo amesema kumekuwa na kero kubwa kwa wanyama hao katika maisha ya watu na kwamba iko haja ya kuangalia namna gani serikali inaweza kuwasaidia wananchi.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa hii ni mara ya pili kwa wabunge wa mkoa wa Kilimanjaro kulalamikia suala la nyani na tumbiri namna inavyowasumbua wananchi ikiwemo watoto wadogo katika kikao cha bumbe hili.