Wapendekeza mshauri wa Rais masuala ya vijana asiwe mzee

Baadhi ya vijana ambao ni viongozi wa vyama vya siasa nchini wakiwa kwenye mkutano wa wabunge vijana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uongozi na siasa jijini Dodoma.
Muktasari:
- Wadau wa masuala ya vijana kwenye uongozi na siasa wamependekeza kuwe na ukomo wa ubunge kama ilivyo kwenye urais ili kutoa na nafasi kwa watu wengine hasa kundi la vijana kuingia kwenye uongozi.
Dodoma. Wadau wanaojishughulisha na masuala ya vijana katika siasa na uongozi wamependekeza kuwepo na ukomo wa nafasi ya ubunge kuwatumikia wananchi pamoja kuwepo na washauri wa rais kuhusu masuala ya vijana wasiwe wazee.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 na mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Ajenda ya Vijana Tanzania, Ocheck Msuva kwenye mdahalo wa kuwasilisha mapendekezo yao kwenye marekebisho ya sheria mbalimbali bungeni.
Msuva amesema kwenye marekebisho ya sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi iweke ukomo wa ubunge kwani wabunge wengi wamekaa madarakani kwa muda mrefu na kuwanyima vijana fursa ya kuwakilisha wananchi.
Amesema katika mapendekezo hayo wabunge wawe na vipindi viwili vya miaka 10 vya kuwawakilisha wananchi badala ya sasa hivi ambapo nafasi hiyo haina ukomo ili kutoa nafasi kwa vijana kugombea nafasi hizo.
“Sisi tunapendekeza kuwe na ukomo wa ubunge, akishatumikia miaka 10 inatosha akae pembeni akafanye mambo mengine awapishe na wengine wawakilishe wananchi maana kwenye nafasi ya urais imewezekana na hata kwa ubunge iwe hivyo,” amesema Msuva.
Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro amependekeza kuwepo na washauri wa rais kuhusu masuala ya vijana wawe vijana wenyewe badala ya wazee.
Amesema washauri hao wakiwa ni vijana watatoa mapendekezo mazuri zaidi kwa kuwa wapo kwenye umri huo badala ya kuwatumia wazee kwenye masuala ya vijana.
Mapendekezo mengine ni kuwepo kwa ushiriki wa vijana kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao watafanya maamuzi na kuziomba mamlaka za uteuzi kuzingatia umri wa vijana kwenye kuteua wajumbe wa tume hiyo.
Aidha ameitaka tume hiyo kuruhusu vijana wenye umri wa miaka 18 kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo mwenyekiti wa serikali za mitaa, udiwani na ubunge kwani kama wanaruhusiwa kupiga kura waruhusiwe pia kugombea kwenye umri huo.
Wamependekeza pia umri wa kugombea Urais uwe ni kuanzia miaka 35 badala ya 40 iliyopo hivi sasa ili kutoa nafasi kwa vijana wengi kugombea nafasi hizo.
Akizungumzia kuhusu marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, mratibu kutoka shirika la Ushirika Tanzania, Raymond Kanegene ametaka asilimia 30 ya viongozi wa juu kwenye vyama vya siasa iwe ni vijana kuanzia mika 35 na endapo mwenyekiti atakuwa na zaidi ya miaka 35 basi makamu wake awe chini ya miaka 30.
“Lengo ni kuwajengea uwezo vijana katika nafasi ya uongozi badala ya kuwatumia kwenye harakati za kiasa na mwisho wa siku wanabaki wakiwa hawana kazi za kufanya,” amesema Kanegene,
Kanegene amesema asilimia 30 ya ruzuku inayoenda kwenye vyama vya siasa itumike kwenye masuala ya vijana ili kuwawezesha vijana hao kuingia kwenye ngazi za uongozi badala ya kusubiri viti maalumu.
Pamoja na hayo wamependekeza kuwe na viti vya vijana bungeni ambao watapigiwa kura na wananchi ili kuleta uwakilishi mkubwa wa vijana bungeni tofauti na sasa wanapoteuliwa kwenye viti maalumu.
Amesema hilo linawezekana kwa sababu kuna baadhi ya nchi za Afrika ambo wamefanikiwa kuwa na nafasi za vijana Bungeni ambao wanawakilisha vijana tofauti na ule uwakilishi wa vijana kutoka kwenye vyama vya siasa.
Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrath Hanje amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 asilimia 70 ya Watanzania ni vijana wenye umri kati ya mika 15 hadi 35 hivyo kama kundi hilo litawekwa pembeni bila kushirikishwa masuala ya uongozi hakutakuwa na viongozi bora wa baadaye.
Amesema yeye anaunga mkono ukomo wa wabunge kuongoza kwa miaka 10 ili wawapishe na watu wengine ikiwezekana hata kwa ngazi ya viti maalum nako kuwe na ukomo ili waende wakagombee majimboni badala ya kuishia nafasi hizo za viti maalumu.