Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mpango: Kutoaminika, rushwa tatizo kwa vijana

Dodoma. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema maadili kwa baadhi ya vijana nchini yameporoka jambo linalowafanya washindwe kuaminika.

“Ni neno lenye ukakasi kulisema lakini ngoja niseme tu, kwamba vijana wengi wa nchi yetu maadili yao yameporomoka, wengi hawana uzalendo na Taifa lao, hawana uadilifu, wavivu na wamejawa na tamaa ya kupata fedha kwa haraka,” alisema Dk Mpango.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kongamano la siku mbili la vijana wa Mkoa wa Dodoma ambalo lilikusanya washiriki 3,500 kutoka wilaya zote saba za mkoa linalofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini hapa.

Lengo la kongamano hilo ni kuwafanya vijana watambue fursa zinazowazunguka na kuzichangamkia ili kujiajiri na kuondokana na hali ya kulalamika kuhusu kukosa kazi.

Dk Mpango alisema kukosa uaminifu kwa vijana kunawafanya washindwe kuijenga Tanzania ya sasa na kesho wakati wanategemewa pindi wazee watakapokuwa wamechoka.

Alisema baadhi ya vijana wamejikita kwenye mambo ya rushwa na utapeli na wengine kwenye mapenzi ya jinsia moja, mambo ambayo ni kinyume na maadili, mila na tamaduni za Kitanzania.

Makamu wa Rais aliwataka vijana kujiepusha na mambo hayo ili walichukue Taifa liwe mikononi mwao kwani wakati ni sasa bila kusubiri kesho.

Hata hivyo, alisema wanaoweza kulichukua Taifa ni wenye maadili mema na kukubarika kwa jamii.

Kwa upande wa Serikali, Dk Mpango aliagiza mambo matano kwa halmashari za wilaya kote nchini, ikiwemo kuwaunganisha vijana katika uzalishaji mali na kuwa na kanzidata za kuwatambua.

Maagizo mengine ni halmashauri kutenga maeneo ya kufanyia biashara na kuyatangaza hadharani, kuwaunganisha vijana na fursa zinazowazunguka kwa uwazi na elimu.

Vijana wenyewe wametakiwa waunde klabu za mazingira ili wasaidie kupambana na uharibifu wa mazingira.

Katika hatua nyingine, Dk Mpango alimwagiza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Deo Ndejembi kuwaandikia barua wakuu wa mikoa kote nchini waige mfano wa Dodoma ili waandae makongamano ya vijana na kuwapa fursa za kujadili mambo yao.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alitaja makundi ya vijana walioshiriki kwenye kongamano hilo kwamba wametoka kwa wajasiriamali, Veta, wanufaika wa mikopo, JKT, Mgambo, bodaboda, machinga na wengine walioko kwenye mafunzo ya miradi ya kilimo ya BBT.

Senyamule alisema vijana watajadili fursa zilizoko mkoani Dodoma ili waweze kuzichangamkia kwa kuwa kila mkuu wa wilaya analo jukumu la kuzungumza kuhusu maeneo yake na mali zilizoko huko, jinsi gani zinaweza kuwa msaada kwa vijana.

Alizitaja baadhi ya mada zitakazofundishwa kwa vijana kuwa ni matumizi ya takwimu, vijana kwa ujenzi wa Taifa la kesho,fursa za uwekezaji, changamkia fursa sasa, afya ya akili na mambo ya mazingira.

Watoa mada katika kongamano hilo Profesa Palamagamba Kabudi, Dk Chris Mauki, Dk Albina Chuwa, Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji), Naibu Waziri wa Tamisemi, Deo Ndejembi na Maida Waziri.

Akizungumza katika kongamano hilo, Ndejembi alitaja changamoto inayowakabiri vijana kwa sasa kuwa ni ukosefu wa mitaji lakini wanapokwenda kuomba mikopo kwenye taasisi za kifedha wanakutana na vikwazo wakitakiwa wawe na dhamana jambo ambalo linawakwamisha.

Ndejembi alitaja kikwazo kingine ni ukopeshaji kuwa wa vikundi ambao unakwamisha baadhi ya watu wanaokuwa wabunifu wakitakiwa kuungana na wengine ndipo wakakope.

Alisema Ofisi ya Rais Tamisemi inakuja na mpango utakaomruhusu kijana mwenye wazo aruhusiwe kukopa mwenyewe.