Waraibu wa dawa za kulevya waomba mikopo isiyo na riba

Kamishina wa kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya (kushoto)akizungumza na vijana walioacha uraibu wa dawa za kulevya ambao kwa sasa wako chini ya uangalozi wa Taasisi ya Organization of Youth Against Risk Behaviors (OYARB) alipotembelea kituo hicho kilichoko Mwendapole Kibaha Mkoani Pwani leo, wapili kushoto ni Mkurigenzi wa Taasisi hiyo, Yohana Kilonzo. Picha na Sanjito Msafiri
Muktasari:
Kamishina wa Kudhiti Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya ameahidi kuendelea kukisaidia kituo hicho kadri iwezekanavyo ili kuwezesha vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya kuishi katika hali nzuri.
Kibaha. Vijana ambao awali walikuwa waraibu wa dawa za kulevya na sasa wameacha tabia hiyo, wameiomba Serikali kuweka mpango utakaowawezesha kupata mikopo ya halmashauri isiyokuwa na riba kama ilivyo kwa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Wamesema kutokana na umri wao kuzidi ukomo wa miaka 35, hawawezi kukopesheka kwa kuwa kifungu cha masharti kinawakataa.
Wametoa kilio hicho leo Alhamisi Desemba 15, 2022 mbele ya Kamishina wa Kudhiti Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya alipotembelea kituo cha kurekebisha waraibu wa dawa za kulevya cha Organization of youth Against Risk Behaviors (OYABI) kilichoko Mwendapole, Kibaha mkoani Pwani.
“Tunakuomba mkuu utusaidie ili sisi vijana ambao tumeacha matumizi ya dawa za kulevya tutengewe fungu maalumu, tuweze kukopeshwa na halmashauri mikopo isiyo na riba ili tujiendeleze kiuchumi,” amesema Emmanuel Msola.
Amesema kuwa mipango waliyonayo kwa umoja wao wanataka kukopa pesa Ili kuanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki hali itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Tukikopeshwa pesa tutakuwa na shughuli za kufanya lakini kama vijana watakuwa hawana kazi walioacha dawa za kuelevya kuna uwezekano wa kurudia tena maana watakuwa hawana kazi za kufanya,” amesema.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Yohana Kilonzo amesema kuwa njia mbalimbali zinazotumika kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya ni pamoja na kuwawezesha kupata ujuzi mbalimbali ikiwemo udereva na ufundi magari.
“Tumewasaidia vijana zaidi ya 20 ambao wamesomea udereva kwa njia ya mtandao kutoka Shirika la Elimu Kibaha lakini changamoto iliyopo ni leseni bado hawajapata kikwazo ni gharama hakuna pesa,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa kata ya Kibaha, Francis Shao amesema kituo hicho kimesaidia vijana wengi kuachana na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na elimu ambayo wamekuwa wakiwapatia kísha kuwaunganisha hospital ya Tumbi kwa ajili ya dawa za methadone.
Kwa upande wake, Kusaya ameahidi kuendelea kukisaidia kituo hicho kadri iwezekanavyo ili kuwezesha vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya kuishi katika hali nzuri.
Amesema hivi sasa ameanza kutembelea vituo vyote vinavyojihusisha na kazi ya kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya ili kuona kama pesa zinazotolewa na Serikali kwenda kwao zinafanya kazi kama inavyotakiwa