Warioba amchambua Mwalimu Nyerere mbele ya Magufuli, Museveni

What you need to know:

Jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere lazinduliwa ramsi, mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo Jaji mstaafu Joseph Warioba azungumzia muasisi alivyokuwa na utu enzi za uhai wake.

Dar es Salaam. Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere nchini Tanzania, Jaji mstaafu Joseph Warioba amezungumzia namna mwasisi wa Tanzania, Julius Nyerere alivyokuwa akiamini utu wa binadamu enzi za uhai wake.

Warioba ametoa kauli leo Ijumaa Septemba 6, 2019 wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo la taasisi hiyo Dar es Salaam, Tanzania.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Rais John Magufuli, Rais wa Uganda  Yoweri Museveni, Mjane wa Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere pamoja na Makamu wa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Pia, Rais wastaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Aman Abeid Karume wa Zanzibar.

Hafla hiyo imekwenda sambamba na kongamano la kumbukizi la Baba wa Taifa Julius Nyerere ambaye alifariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London nchini Uingereza.

Warioba ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania ametoa kauli akizungumza kwa niaba ya bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo, akisema Mwalimu Nyerere aliamini binadamu wote ni sawa na wanastahili heshima.

“Ndiyo maana yeye na waasisi wenzake wa Taifa hili, walianzisha haraka za kupata uhuru, kisha kuzisaidia nchi nyingine za Afrika. Aliamini umoja na mshikamano ni nguvu na msingi wa amani.” 

“Yeye na waasisi  Abeid Aman Karume (Rais wa kwanza wa Zanzibar) wenzake walijenga umoja, mshikamano pamoja na kuunda muungano na kujenga Taifa lenye amani bila ubaguzi. Mwalimu alikuwa mwadilifu, mcha Mungu, mzalendo na mwenye nidhamu ya hali ya hali juu,” amesema Warioba.

Warioba amesema Mwalimu Nyerere aliamini katika maendeleo ya watu, kwake maendeleo hakuhesabu  kama ni fedha bali aliamini yataonekana endapo kila mtu anapata chakula bora cha kutosha, makazi mazuri na anavaa vizuri, kupata majisafi na salama

“Haya mambo hakuyabuni bali ni ya msingi kwa maisha, binadamu wakati wote na dunia nzima. Mwalimu alichofanya ni kutuachia urithi wa kuyaenzi,” amesema Warioba.