Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Warioba, Mkuchika waongeza nguvu Tume Haki Jinai

Muktasari:

  • Tume ya kurekebisha mifumo ya haki jinai, imeongezewa nguvu ikiwa katika hatua ya kusaka mbinu za utekelezaji wa mapendekezo yake.

Dar es Salaam. Jaji mstaafu Joseph Warioba na Kapteni George Mkuchika wameteuliwa kuongeza nguvu katika timu ya wajumbe 11 wa tume ya kurekebisha mifumo ya haki jinai.

Uteuzi wa wawili hao, unaifanya tume hiyo iliyoundwa Januari 31, mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa na jumla ya wajumbe 13, badala ya 11 wa awali.

Hata hivyo, nyongeza ya wajumbe hao imefanywa na Rais Samia wakati tume hiyo ikiwa katika hatua ya mchakato wa kujadili mbinu za utekelezaji wa mapendekezo hayo.

Uteuzi wa wawili hao, umedokezwa leo Novemba 8, 2023 na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Othman Chande, wakati tume hiyo ilipowasilisha ripoti yake kwa mabalozi na mashirika ya kimataifa.

Akisoma muhtasari wa mapendekezo ya tume hiyo, Jaji Chande amesema katika hatua iliyofikiwa, Rais Samia amewateuwa wawili hao kuongeza nguvu.


"Katika awamu hii ya utekelezaji, Rais Samia  amemteua Jaji mstaafu Joseph Warioba na Kapteni George Mkuchika kuwa sehemu ya tume, akijua hawa ni watu mahiri na viongozi wenye uzoefu katika masuala haya," amesema.

Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, amewahi kuziongoza tume mbalimbali ikiwemo ile iliyoundwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Tume nyingine, iliyowahi kuongozwa na mtaalamu huyo wa sheria ni ile iliyoundwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete mwaka 2014 ya kurekebisha Katiba.

Mkuchika, ndiye mwanasiasa anayetajwa kuwahi kuhudumu karibu katika Serikali zote nchini, tangu awamu ya kwanza.

Katika kipindi hicho chote, Mkuchika ameshika nafasi mbalimbali za kisiasa ikiwemo ubunge, uwaziri na mkuu wa mikoa mbalimbali.

Miongoni mwa wizara alizowahi kuziongoza no Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), lakini sasa ni Waziri katika Ofisi ya Rais, asiye na Wizara Maalumu.

Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue amesema baada ya kukamilisha ripoti Rais Samia amebadili tume hiyo kwa kuunda kamati mbalimbali za kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo.

Kinachofanywa sasa, amesema ni kumsaidia Rais kutengeneza njia za utekelezaji wa mapendekezo hayo.

"Kwa sasa tunahusisha taasisi mbalimbali kupokea ushauri wao juu ya utekelezaji na hii ni wiki ya tatu tunafanya," amesema.

Ameeleza baada ya hatua hiyo watapendekeza kipi kinapaswa kutekelezwa kwa muda mfupi, wa kati na mrefu kisha watapendekeza kujua nani atafanya nini.

Kulingana na Balozi Sefue, baadaye watakaa kikao cha makundi mbalimbali na kila moja litapewa kazi ya kufanya na halitatakiwa kutoka bila mapendekezo ya utekelezaji.

Jukumu lao, amesema ni kuhusisha washirika mbalimbali ili kujifunza kutoka katika uzoefu wa nchi zao.

"Naamini kila nchi ina njia zake ilizokuja nazo kufanya maboresho ya sera na sheria kuhusu mifumo ya haki jinai," amesema.

Balozi Sefue ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, ameeleza milango ipo wazi juu ya kuwajengea uwezo wajumbe hao kuhakikisha kunakuwa na rasilimali na msaada wowote wa kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo.