Wasio na bima ya afya kukosa baadhi ya huduma ifikapo mwaka 2026

Muktasari:

  • Mjumbe wa sekretatieti ya bima ya afya kwa wote kutoka Wizara ya Afya, Jackline Tarimo amesema ikifika mwaka 2026, watu wote wasiofanya kazi katika sekta rasmi, watakapohitaji huduma mbalimbali kutoka taasisi za umma watatakiwa kuonyesha kadi ya bima ya afya kwa wote.

Mwanza. Serikali imesema muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ukipitishwa na kuwa sheria na kuanza kutumika mwaka huu, mwananchi yoyote ambaye hatakuwa na bima hiyo kuanzia mwaka 2026, hataweza kupata huduma zingine ikiwamo leseni ya udereva.

 Kauli hiyo imetolewa leo na mjumbe wa sekretatieti ya bima ya afya kwa wote kutoka Wizara ya Afya, Jackline Tarimo wakati akitoa mada kwenye kikao cha  wadau wa afya mkoani Mwanza kilicholenga kufanya tathmini ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote.

Tarimo amesema ukifika muda huo watu wote wasiofanya kazi katika sekta rasmi, watakapokuwa wanahitaji huduma mbalimbali kutoka taasisi za umma watatakiwa kuonyesha kadi ya bima ya afya kwa wote.

“Ikifika mwaka 2026, mtu akienda kupata huduma muhimu sehemu kama vile kukata leseni ya udereva pamoja na wanafunzi wanaoanza vyuo vikuu, watatakiwa kuonyesha kadi ya bima ya afya,” amesema.

Amesema lengo la serikali kufanya hivyo siyo kuwatesa wananchi wake bali kufanya upatikanaji wa huduma ya afya kwa wote kuwa kipaumbele kwa wananchi.

Hata hivyo, amesema baada ya kutungwa sheria hiyo kabla ya mwaka 2026, haitakuwa lazima kwa wananchi wote kukata bima hiyo hadi pale muda wa matazamio utakapomalizika, ndipo itakuwa lazima kwa kila mwananchi kuwa nayo.

Ukamilishwaji wa muswada wa sheria wa bima ya afya kwa wote unatarajiwa kufanyika katika vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza karibuni Bungeni Dodoma baada ya muswada huo kuachwa kiporo mwaka jana.

Kuhusu wasiyojiweza, Jackline amesema serikali imetenga fedha na kuandaa utaratibu utakaosaidia kuwatambua watu wasioweza kulipia gharama za bima hiyo ikiwa ni pamoja na kutumia taarifa za Tasaf kuwatambua wasiojiweza.


Katika hatua nyingine, serikali imetoa onyo kwa vituo vikubwa vya kutolea huduma za afya ambavyo vinafanya utapeli wa gharama halisi za matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF).

Akizungumza na wadau wa sekta ya afya wakiwamo wauguzi na waganga wakuu wa mikoa na halmashauri za wilaya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa, Abel Makubi amesema serikali itavifungia vituo vinavyofanya utapeli wa gharama za matibabu.

Profesa Makubi amesema vituo vyote ambavyo vimeingia mkataba na NHIF vihakikishe vinafuata miongozo na mkataba waliosaini huku akiuagiza mfuko huo kulipa fedha za matibabu ndani ya siku zisizozidi 15 tangu kulipwa fedha hiyo na serikali.

“Hatutasita kuvifungia vituo vyote ambavyo vitafanya udanganyifu wa aina yoyote wa gharama ya matibabu ya mgonjwa aliyotumia. Mtalalamika sana ila sisi tumeshawafunga,” amesema.

Profesa Makubi amewaagiza watoa huduma za afya kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa wote bila kuchoka ili kuongeza mwamko wa wananchi kutoka sekta isiyo rasmi kujiunga na bima hiyo mara baada ya muswada wa bima hiyo kupitishwa.