Wataalamu wa afya Tanzania, Uingereza kubadilishana ujuzi
Muktasari:
- Katika uboreshaji wa huduma za afya nchini, wataalamu wa Tanzania na Uingereza, watatembeleana kujifunza namna matibabu yanavyotolewa na wataalamu kutoka nchi hizo mbili.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea ametaja vipaumbele vitatu vya ushirikiano baina ya watalamu wa afya Tanzania na Uingereza, huku utafiti kwenye eneo la tiba ukipewa kipaumbele.
Eneo lingine ni uimarishaji wa huduma za tiba ambapo wataalamu wa afya nchini tayari wamekutanishwa na madaktari bingwa kutoka nchini Uingereza. Pia, kujengeana uwezo baina ya wataalamu hao nalo litakuwa kipaumbele.
Akizungumza kwenye kongamano kati ya wataalamu wa Tanzania na Uingereza lililofanyia jana Juni 21, 2024, Dk Nyembea amesema lengo ni utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2023 na nchi hizo mbili kwenye sekta ya afya.
Amesema wataalamu wa Tanzania na Uingereza watabadilishana mawazo jinsi sayansi ya matibabu inavyotekelezwa baina ya mataifa hayo mawili.
“Maeneo ya ushirikiano yaliyolengwa ni kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini na huku kutakuwa na mambo yatakayotekelezwa, tunategemea kuona uwekezaji wa kigeni hasa kwenye sekta ya afya hasa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba na hili eneo ni muhimu kwa sababu tayari tuna rasilimali watu ambao wamesoma,” amesema.
Kufutia kongamano hilo, Dk Nyembea amesema matarajio makubwa yaliyopo ni kuboreshwa kwa huduma za tiba na hiyo ndio ajenda ya nchi.
Kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema kongamano hilo ni moja ya matokeo ya makubaliano waliyoingia Tanzania na Uingereza kwenye sekta ya afya.
“Tunategemea kushirikiana na wenzetu kutoka Uingereza kwenye matibabu ya upasuaji wa ubongo, tiba ndani ya ubongo, figo na utafiti,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema wagonjwa wengi wanalazwa vyumba vya uangalizi maalumu wakiwa kwenye hali mbaya na kupoteza maisha kutokana na kuchelewa kwa huduma.
Kutokana na hayo, Dk Kisenge amesema wamekubaliana na wataalamu kutoka Uingereza, kuwasaidia miongozo ya kupunguza vifo vya watu waliozidiwa.
“Pia watatusaidia kufundisha madaktari wetu namna ya kuhudumia wagonjwa walio mahututi, kwa upande wa moyo, watatusaidia kwa wale wagonjwa waliopata mshtuko wa moyo wa ghafla. Uingereza wana mfumo mzuri wa kuhudumia wagonjwa hawa kwa kupata huduma ndani ya dakika 30,” amesema.
Amesema kwa Tanzania, wagonjwa hao wanaweza kupata huduma ndani ya saa moja au saa 24 kutokana na umbali, hivyo sekta ya afya itaiga mfumo wa matibabu wa Uingereza.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Laurient Mchome, amesema watajifunza namna namna mpya ya utoaji matibabu kutoka Uingereza katika huduma wanazotoa za upasuaji.
“Tutaangalia namna ya kutatua changamoto zilizopo kwenye utendaji wetu chini ya mwongozo wa Wizara ya Afya ili tutoe huduma bora kwa wananchi. Kwenye afya mambo mapya yanatokea ikiwemo mabadiliko ya teknolojia, hivyo mkutano huu ni muhimu kubadilishana ujuzi,” amesema.
Teknolojia mpya ya matibabu ya kiharusi ndiyo matarajio ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi anayeeleza kwamba mgonjwa wa kiharusi anaweza kupona kabisa akiwahi matibabu.
“Kutupa hela au kifaa si kwamba haitusaidii lakini ukitupa utaalamu kutakuwa na faida nyingi, mfano ukimleta mtalaamu wa kiharusi kutoka Uingereza atafundisha watu wengi kwa wakati mmoja kwenye mazingira yetu sisi, pia tunabadilishana maarifa na hawa wenzetu yapo magonjwa Uingereza hayapo yapo nchini kwetu,” amesema.
Diaspora anayefanya Hospitali ya Queens ya Uingereza, Profesa Gideon Mlawa amesema tayari wameanza kutembelea hospitali mbalimbali zilizopo hapa nchini kujifunza na kutoa ujuzi walionao.
“Nchini Uingereza, mgonjwa mmoja anaweza kuwa anaangaliwa na timu ya wataalamu mbalimbali, kuanzia mpishi, mfanya usafi na madaktari, tumeshauri kuwe na timu ya kumhudumia mgonjwa ili kumharakishia mgonjwa matibabu,” amesema.