Wataalamu watoa tahadhari kwa makundi haya kabla ya chanjo

Tahadhari kwa makundi haya kabla ya chanjo

Muktasari:

  • Wakati chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 ikiendelea kutolewa nchini kwa watu mbalimbali, wataalamu wa afya wamesema mtu anayeumwa na watoto wenye umri chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kupata chanjo hiyo.

Dar es Salaam. Wakati chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 ikiendelea kutolewa nchini kwa watu mbalimbali, wataalamu wa afya wamesema mtu anayeumwa na watoto wenye umri chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kupata chanjo hiyo.

Makundi hayo yameelezwa na wataalamu wa afya wanaofanya kazi na Ubalozi wa Marekani nchini wakati wa mkutano wa maswali na majibu kwa waandishi wa habari kuhusu chanjo hiyo.

“Watoto chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kupata chanjo ya Covid-19 kwa sababu utafiti wa chanjo hizo haukujikita kwa watu wa rika hilo ...pia mtu anayeumwa asichanje asubiri mpaka upone,” alisema Dk Arkan Ibwe, anayetoa huduma za matibabu kwa raia wa Marekani wanaojitolea katika maeneo mbalimbali.

Dk Ibwe ambaye ana uzoefu wa miaka 10 akijikita zaidi katika huduma za matibabu, alisema watu wengine hawatakiwi kuchanjwa ni watu wenye mzio (allergy), lakini kwa kushauriana na madaktari wao wanaweza kufanya hivyo.

“Unakuta mtu mwingine mwili wake una shida na vitu vinavyotumika kutengeneza chanjo hiyo, si vema akachanja bila kushauriana na daktari kuona iwapo kilichotumika kutengeneza chanjo hiyo hakina madhara kwake,” alisema.

Pamoja na hayo, Dk Ibwe alisema kwa watu wenye magonjwa ya muda mrefu chanjo ni muhimu, lakini ni vema akashauriana na daktari anayemhudumia ili ampe ushauri bora.

Alieleza pia hata wajawazito wanapaswa kwanza kushaurina na madaktari wao kabla ya kuchanjwa, huku akisisitiza kuwa hao ni miongoni mwa watu wa mstari wa mbele kupata chanjo kutokana na kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi kwa urahisi.

“Hakuna kitu kinazuia mjamzito asipate chanjo kwa sababu ya mabadiliko ya mwili wake, yupo kwenye kundi la kupata Covid kali, anastahili kupata kinga, ni vema akashauriana na daktari wake,” alisema.

Akizungumzia uwepo wa chanjo nyingi na kuijua iliyo bora, Dk Eva Matiko ambaye ni bingwa wa afya ya jamii alisema chanjo inayostahili ni ile inayopatikana kwa haraka katika eneo husika ikiwa salama kwa matumizi, ili kuokoa watu na majanga kama ya Covid-19.

“Wakati wa janga WHO (Shirika la Afya Duniani) hutoa idhini ya dharura ya matumizi ya dawa na vifaa tiba, kinachozingatiwa ni ubora na usalama. Kila Taifa huchagua bidhaa kwa kuangalia hali ya hewa ya sehemu kubwa ya nchi, uwezo wa uhifadhi kutoa na kusambaza,” alisema Dk Matiko, mwenye uzoefu wa miaka 20.

Naye Dk Emmanuel Tluway anayefanya kazi ya Usaid akizungumzia kuhusu chanjo hiyo kupatikana mapema, alisema sasa kuna maendeleo ya teknolojia na mataifa makubwa na matajiri duniani wamewekeza nguvu kubwa kuhakikisha wanapata suluhisho la ugonjwa huo.

“Tofauti na magonjwa mengine ambayo yalionekana ni ya watu fulani, Covid-19 ilionekana haibagui inashika yeyote, hivyo suluhisho lake limeungwa mkono na watu wengi. Matajiri wameweka fedha ili kupata suluhu, vilevile watu wa majaribio waliojitoa sana na mapema,” alisema Dk Tluway.

Katika mkutano huo, Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright alisema chanjo hiyo imeleta matokeo chanya katika taifa lake ambalo mpaka sasa ndilo limerekodi kiwango kikubwa cha maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

“Sayansi haina hofu kuhusu suala hili, hivi sasa nchini Marekani zaidi ya asilimia 99 ya vifo vipya vinavyotokana na Covid-19 ni watu ambao hawajachanja, ukweli mwepesi ni kuwa chanjo hizi zinaweza kuokoa maisha yako na mpendwa wako,” alisema Dk Wright.

Balozi huyo ambaye ni daktari wa binadamu alisema maamuzi ya kitabibu ni miongoni mwa maamuzi muhimu na chanjo zimekuwa nyenzo muhimu ya kulinda afya ya jamii kwa zaidi ya miaka 200 sasa.

Hata hivyo, ubalozi huo ulisema chanjo ya J&J ambayo ilitoa kama msaada hapa nchini haitumiki sana Marekani kwa kuwa ilichelewa kutengenezwa na kuidhinishwa, hivyo ikakuta dawa nyingine zimeshaliteka soko kubwa la raia wa taifa hilo kubwa duniani.