Watahadharishwa matumizi holela ya chanjo

Muktasari:

Daktari Mwakapeje amesema usugu wa vimelea unaweza kuhama kutoka kwenye mifugo na kwenda kwa binadamu na pia unaweza kutoka kwenye viumbe hai kama wanyama na binadamu na viumbe wengie na kwenda kwenye mazingira.

Mbeya. Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula (FAO) limetahadharisha jamii ya wakulima na wafugaji kuzingatia ushauri wa kitalaam kabla ya kununua na kutumia dawa yoyote kwa matumizi ya binadamu, mifugo, kilimo na kwenye mazingira kuepuka usugu wa vimelea.
Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mratibu wa mradi wa kuthibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa wa shirika hilo, Dk Elibariki Mwakapeje.
Akizungumza na wananchi waliotembelea banda la FAO katika maonesho ya Nanenane yaliyomalizika hivi karibuni jijini Mbeya, mratibu huyo amesema jamii ya wakulima na wafugaji ni muhimu wakaelewa matumizi sahihi ya dawa ili kukomesha au kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa.  
“Tunawaelimisha wananchi kwa sababu usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ni ile hali inayotoea baada ya dawa zilizokuwa zikifanya kazi siku za nyuma zinakuwa hazifanyi kazi sawa sawa,” amesema.
Daktari Mwakapeje amesema kuwa sababu nyingine zinatokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa maana kwamba pengine dawa inakuwa siyo sahihi kwa magonjwa yanayokuwa yamelengwa au matumizi sahihi ya dozi.
Kadhalika anasema usugu wa vimelea unaweza kuhama kutoka kwenye mifugo na kwenda kwa binadamu lakini pia unaweza kutoka kwenye viumbe hai kama wanyama na binadamu na viumbe wengie na kwenda kwenye mazingira.
Naye Dk Gibonce Kayuni kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi amewaasa wakulima na wafugaji kufuata kanuni za ufugaji bora (biosecurity) na masharti ya chanjo
Akitolea mfano amesema kuweka dawa mahali pasipostahili baadhi ya wadudu wanaweza kuendelea kula kidogo kidogo na hatimae dawa hiyo ikageuka kuwa sugu.
“Mdudu huyo akizoea dawa anaweza kushindwa kuuwawa na dawa hiyo na kuongeza gharama kwa mfugaji au mkulima kununua dawa nyingine,” amesema