Wataka matukio ya ukatili yadhibitiwe, Beatrice akizikwa
Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakiwa wamebeba jeneza lililobeba mwili wa Beatrice Minja (47) anayedaiwa kuchomwa visu 25 sehemu mbalimbali za mwili wake na mpenzi wake. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Beatrice aliyezikwa leo nyumbani kwao katika Kijiji cha Mbomai wilayani Rombo, alichomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na mpenzi wake, Lucas Tarimo, Novemba 12, 2023 kabla ya kufariki Desemba 27 akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Rombo. Wakati mamia ya wananchi wakishiriki maziko ya Beatrice Minja (47) anayedaiwa kuuawa na mpenzi wake kwa kumchoma kisu mara 25, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, viongozi wa dini, wanajamii wameiomba Serikali kuongeza nguvu ya kudhibiti matukio ya ukatili katika jamii.
Beatrice aliyezikwa leo nyumbani kwao katika Kijiji cha Mbomai wilayani humo, alichomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na mpenzi wake, Lucas Tarimo, Novemba 12, 2023 kabla ya kufariki Desemba 27 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo, Tarimo alikamatwa Desemba 31 alfajiri akiwa amejificha kijiji cha Jema, kata ya Oldonyosambu, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha na akidaiwa kunywa sumu na Januari 1, 2024 alifariki.
Leo Januari 3,2024 katika mazishi ya Beatrice, Wakili wa Parokia ya Mtakatifu Pius wa X-Tarakea, Jimbo Katoliki la Moshi, Padre Timotheo Mwanda amesema asilimia 90 ya matukio ya ukatili yanayotokea katika jamii yanafanywa na ndugu na wakati mwingine watu wanaofahamiana, hivyo akawataka wanajamii kuyachukia.
"Beatrice, ni mama aliyekuwa akiwajibika na kujituma kweli kweli, hakuwa akitgemea nguvu za mtu mwingine, alikuwa ni mpambanaji na mcha Mungu, wengi tulimfahamu kwa uchapakazi wake,” amesema.
Amesema alipigiwa simu na kujulishwa kuwepo kwa tukio la kikatili kwa Beatrice, jambo lililomuumiza kwa kuwa alikuwa akimfahamu marehemu.
“Asilimia 90 ya haya matukio yanafanywa na watu wetu wa karibu, ninapoangalia kifo hiki katika roho ya imani ni kwamba amani ulimwenguni imepungua, hata ukiangalia leo tunasikia makanisa na misikiti inachomwa, watu wameuawa," amesema.
Kwa upande wake Mbunge mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki, Pamela Maasay amesema matukio ya namna hiyo sio mara ya kwanza kutokea kwenye jamii na kuwaomba viongozi waliopewa dhamana na Serikali kuyadhibiti.
"Hili sio tukio la kwanza kutokea katika kijiji chetu cha Mbomai, yameshatokea ya kutisha inawezekana zaidi ya hili, kumekuwa na mtiririko wa muda mrefu sana wa matukio ya ajabu na yakuogofya.
“Hiki kilichompata ndugu yetu Beatrice kuna uwezekano kwamba ni matokeo ya namna ambavyo sisi tumekuwa tukiishi kwenye jamii zetu,” amesema.
Ameiomba Serikali kuja na mkakati maalumu wa kuponya majeraha kwa jamii au familia zilizopoteza ndugu zao.
Naye Kamishna Msaidizi wa Jeshi la polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi nchini, Ralph Meela ameitaka jamii kutoa taarifa kwenye vyombo husika pale ambapo wanaona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.
"Ifikie mahali sio kwamba uliyenaye karibu ni salama sana kwako, pale utakapoona kuna viashiria vyovyote vile vya mtu kuonyesha dalili za kutenda kosa lolote baya, usije kuishia kusema tu huyu ni mpenzi wangu, mume wangu, mke wangu hapana, toa taarifa kwa watu ambao wanaweza kukusaidia.
"Sasa hivi Jeshi la Polisi lipo kila mahali tuna wataalamu wetu wa ustawi wa jamii wapo na wanaweza kuwasaidia, tusijichukulie sheria mkononi kama ilivyotokea, hatukutegemea kuwepo hapa leo lakini tukio kama hili limetufikisha hapa," amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Rombo, Felichism Oisso, amesema tukio hilo walilipokea kwa masikitiko makubwa na kulaani vikali mauaji hayo ya kikatili, wakiahidi kuwa wapo pamoja na familia katika kipindi kigumu cha maombolezo.
Akisoma historia ya marehemu, ndugu wa familia hiyo, Anselim Mkonyi amesema familia imepata pigo kubwa kwa kifo cha dada yao kwa kuwa ni mtu ambaye alikuwa akitegemewa.