Watanzania waibuka kidedea mbio za Kili Marathon

Muktasari:
- Simbu alimaliza katika muda wa 02:16:31 akifuatiwa na Wakenya Anold Kiptaoi na James Tallam, waliomaliza nafasi za pili na tatu katika muda wa 02:17:05 na 02:17:43.
Wanariadha wa Tanzania leo Jumapili Februari 27, wameitoa taifa kimasomaso katika mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika jana mkoani Kilimanjaro, huku Aloyce Simbu akishinda kilomita 42 za mbio hizo.
Kwa upande wa km 42, Kenya kwa miaka mingi imekuwa ikitawala mbio hizo, lakini safari hii Simbu ambaye ni mdogo wa mkimbiaji wa kimataifa Alphonce Simbu amevunja mwiko huo.
" Najisikia furaha sana kushinda, nilijaribu mwaka 2018 lakini niliishia kilomita 35 tu sikumaliza kilomita zote 42," amesema Simbu.
Simbu alimaliza katika muda wa 02:16:31 akifuatiwa na Wakenya Anold Kiptaoi na James Tallam, waliomaliza nafasi za pili na tatu katika muda wa 02:17:05 na 02:17:43.
Katika upande wa wanawake wa mbio za km 42 za Kilimanjaro Premium Lager, Mkenya Shelmith Muriuki ameshinda kwa muda wa 02:41:06 na nafasi ya pili pia ilikwenda kwa Mkenya mwenzake Flavious Kwamboka akimaliza muda wa 02:57:22. nafasi ya tatu alishinda Mtanzania Angel John ( 03:06:13)
Katika mbio za Tigo ( km 21), Mtanzania Emmanueli Giniki ameibuka mshindi kwa muda wa 01:00:35 huku Watanzania wengine, Gabriel Geay na Inyasi Sulley wakimaliza nafasi za pili na tatu katika muda wa 01:02:05 na 01:04:11.
Kwa upande wa wanawake, Mkenya Agness Ngolo alishinda kwa muda wa 01:12:17 na Watanzania Jackline Sakilu na Natalia Elisante wakimaliza nafasi za pili na tatu katika muda wa 01:14:50 na 01:15:07.
Akizungumza kabla ya kutoa medali kwa washindi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasifu waandaaji na wadhamini wa michuano ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa kushirikisha zaidi ya wakimbiaji 12,000 kutoka nchi zaidi ya 58 duniani.
"Nimeshuhudia watu wengi sana wakati naanzisha mbio za kilomita 5 za Grand Malt, 21 za Tigo na 42 za Kilimanjaro Premium Lager, huo haijapata kutokea,"amesema Waziri Mkuu.
" Kwa ukubwa huu, mnapaswa kuitwa Kilimanjaro International Marathon, maana watu ni wengi kutoka nchi mbalimbali," amesema Waziri Mkuu.
Pia amewasifu wadhamini kwa kuyafanya kuwa mashindano makubwa kuliko yote hapa nchni,".
Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2022 ni Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu) Tigo (21km) na Grand Malt (5km).
Wadhamini wa meza za maji ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC Sugar, Simba Cement na Kilimanjaro Water. Wasambazaji rasmi ni GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles na Surveyed Plots Company Ltd (SPC) na Bodi ya Utalii (TTB).
" Najua kuna mbio nyingi za marathon, lakini hizi za za Kilimanjaro Marathon ni baba yao," amesema.
Wakiongea katika mbio hizo, Mkurugenzi wa TBL, Jose Moran amesema wanajisikia furaha kubwa sehemu ya mafanikio ya mbio hizo kwa miaka 20 ya udhamini wao.
Pia Kaimu Mtendaji wa Kampuni ya Tigo Tanzania , Innocent Rwetabura amesema Tigo imekuwa ikidhamini mbio za kilomita 21 tangu mwaka 2015 kwa mafanikio.
Pia amemwambia Waziri Mkuu kuwa Tigo inashiriki kampeni ya upandaji miti katika mlima Kilimanjaro ili kuendeleza uwekaji wa mazingira.
Simba amepata milioni 4.1 kama zawadi kuu, na pia m1.5 kama bonasi na kiwanja kigamboni . Washindi wengine pia wamepewa pesa taslimu.