Watanzania watakiwa kuyaenzi aliyofanya Magufuli
Hayati John Magufuli
Muktasari:
Watanzania wametakiwa kuendelea kuyaenzi mema aliyoyafanya Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli wakati wa uhai wake.
Chato. Watanzania wametakiwa kuendelea kuyaenzi mema aliyoyafanya Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli wakati wa uhai wake.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Afican Inland Church (AIC) Jimbo la Geita, Musa Magwesela leo Alhamisi Machi 17, 2022 kwenye uwanja wa Magufuli Chato wakati wa kuadhimisha kumbukizi ya mwaka mmoja ya kifo cha hayati Magufuli akisema hayati Magufuli ameacha alama ambayo haitafutika mioyoni mwa Watanzania.
Amesema wakati wa uhai wake hayati Magufuli alikua mcha Mungu aliyejitoa kujenga misikiti na makanisa bila kujali dini yake.
Amesema Magufuli alihubiri uzalendo na alikua na uthubutu uliosaidia miradi mikubwa ya kiuchumi kujengwa huku akiweka mbele maslahi ya wananchi wanyonge.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel ambaye wakati wa uhai wa Magufuli alikua Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema hayati Magufuli atakumbukwa kwa mema na hatasahaulika kwa kuwafundisha Watanzania kuwa wazalendo na kuipenda nchi yao.
Wananchi wakiwa kwenye uwanja wa Magufuli mjini Chato wakisubiri ibada ya misa takatifu kuanza.
Amesema wakati wa uhai Wake Magufuli alitaka viongozi kutumia maarifa na kutekeleza majukumu yao kwa upendo zaidi.
“Tunakumbuka mema aliyoyafanya ni faraja kwa Watanzania alitufundisha kuwa wazalendo kuleta tija na kusema ujenzi wa daraja la Busisi ni miongoni mwa alama ambayo haitasahaulika kwa wananchi hasa wa mikoa ya Geita na Mwanza” amesema.
Tangu asubuhi wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo wastaafu walianza kuingia kwenye uwanja huo wa Magufuli kuhudhuria maadhimisho hayo.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hassein Mwinyi na mkewe pamoja na makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Philip Mpango.
Wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson, Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula, Waziri wa Tamisemi, Inocent Bashungwa, Mbunge wa Jimbo la Ismani, William Lukuvi pamoja na Balozi Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole.
Pia wapo viongozi wastaafu wakiwamo Makamu wa Rais wa awamu ya nne, Ghalib Bilali, mawaziri wakuu wastaafu Joseph Warioba na Mizengo Pinda.
Wengine ni aliyekuwa Spika wa Bunge, Anna Makinda mke wa Rais wa awamu ya tatu hayati, Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa.
Tayari familia ya hayati Magufuli ikiongozwa na mkewe, Janeth Magufuli ipo uwanjani kushiriki ibada ya misa hiyo.
Kwa sasa anayesubiriwa kuwasili ni anaesubiriwa sasa ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa ratiba, maadhimisho hayo yatatanguliwa na ibada ya misa takatifu itakayoongozwa na makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kasala na baada ya ibada utafuatia utambulisho na salamu kutoka kwa wawakilishi mbalimbali.
Baada ya salamu Rais, viongozi pamoja na familia wataambatana kwenda kwenye kaburi la Hayati Magufuli kwa ajili ya kuweka mashada ya maua.
Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu, mwili wake ulizikwa Ijumaa Machi 26, 2021 katika kijiji cha Mlimani wilayani Chato Mkoa wa Geita katika makaburi ya familia. Â