Watanzania zaidi ya 300 kupandisha bendera Mlima Kilimanjro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya twenzetu kileleni, kupandisha bendera ya Taifa kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika.
Muktasari:
- Zaidi ya Watanzania 320 kutoka sehemu mbalimbali nchini wanatarajiwa kupandisha bendera ya Taifa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika Desemba 9.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka Watanzania watakaopanda mlima kilimanjaro kupitia Kampeni ya 'Twenzetu kileleni' katika maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika kuhakikisha kila mmoja anapanda mti lengo likiwa ni kurejesha uoto wa asili pamoja na barafu ya mlima huo ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika.
Babu ametoa rai wakati wa uzinduzi wa kampeni ya 'Twenzetu Kileleni' iliyofanyika katika Hoteli ya Springlands iliyopo Manispaa ya Moshi, ambapo zaidi ya Watanzania 320 wanatarajiwa kupandisha bendera ya Tanzania katika kilele cha Uhuru ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika.
Amesema barafu katika mlima huo imepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi hivyo zinahitajika jitihada za makusudi za pamoja za kupanda miti kwa wingi ili kurejesha uasili wa mlima huo.
"Ndugu zangu Mlima Kilimanjaro miaka ya nyuma ukiutizama wakati mawingu hayapo ulikuwa umejaa barafu yakutosha mpaka chini lakini leo barafu imekuwa ni vipande vipande kwa sababu tunaharibu mazingira, hivyo tumedhamiria kurudisha ukijani wa Kilimanjaro kwa kupanda miti," amesema RC Babu.
"Tutaungana katika kampeni hii kuhakikisha tunapanda miti kila anayekuja kwenye nchi yetu tumwombe apande mti, awe mtalii wa kutoka nje au Tanzania apande miti na hawa watu 320 wanaopanda mlima Kilimanjaro siku ya maadhimisho ya maka 62 ya uhuru ambao wataanza kupanda Desemba 3 mwaka huu, kila mmoja abebe mti wake," amesema.
"Tunautegemea mlima huu katika kuongeza mapato ya nchi yetu na kuwezesha serikali kufanya shughuli zake, Kinapa na Tanapa ni muhimu mkasimamia masuala ya mapato na nitoe wito kwa Watanzania kupanda mlima ili kuchochea maendeleo ya mkoa wetu," amesema.
"Nitoe wito kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, viongozi na Watanzania wote kuja kuunga mkono kampeni hii ya 'twenzetu kileleni' kusherekea miaka 62 ya uhuru wa nchi yetu, miaka 62 ni mingi sana, ni lazima tuenzi uhuru wetu," amesema.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Zara Adventures, Zainabu Anselim amesema wao kama wadau wa utalii nchini wamekuwa wakaihamsisha na kuhakikisha kila mtalii anayepanda Mlima Kilimanjaro anapanda mti ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu yake hatua ambayo inachochea uhifadhi wa mazingira ya mlima huo.
"Katika kampeni ya mwaka huu ya kupandisha bendera kilele cha Uhuru tutaanza na shughuli ya kupanda miti kabla ya kupanda mlima ili tuweze kuonyesha kuwa tunaweza kulinda na kuhifadhi uasili wetu kwani miti inaweza kutusaidia kutunza mazingira yetu," amesema.
"Ni baraka kubwa kwetu sisi wananchi wa mkoa huu kuweza kuwa na mlima kama huu, tunaomba kuhamasisha Watanzania wote tushirikiane pamoja tuweza kupanda mlima kuadhimisha miaka 62 ya uhuru tukijivunia umoja na mshikamano wetu," amesema.
Ofisa Uhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), Gladys Ng'umbi amesema zoezi hilo ambalo litaanza Desemba 3 litashirikisha njia tatu za kupanda mlima Kilimanjaro ambazo ni Marangu, Machame na Lemosho.
Amesema kila Mtanzania anapaswa kujivunia vivutio vilivyopo ikiwemo kuhamsishana kupanda mlima huo ili kuutangaza katika mataifa mbalimbali katika maadhimisho hayo ili kuleta umoja na mshikamano kwa Watanzania wote.
"Twende tukaadhimishe miaka 62 ya uhuru wetu kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro ambacho ni kilele kirefu kuliko vyote barani Afrika, niwahakikishie Watanzania kwamba tumejipanga kwa kushirikiana na kampuni za kitalii na wadau wengine kutoka kwenye taasisi pamoja na serikali kuhakikisha watakaopanda mlima watapata huduma zenye ubora unaotakiwa," amesema
Dk Abednego Mashambo, kutoka Shirika la uokoaji la Kili Med Air, amesema shirika hilo limejipanga kuhakikisha wale wote watakaopata changamoto za mlima wanapata huduma za haraka.
"Tumejipanga kwa wale watakaopata shida katika mlima wetu watakuwa na matibabu maalum ambapo wataweza kuendelea na safari, kwa hiyo tumejipanga lakini kwasababu namba imeongezeka zaidi tutaongeza idadi ya madaktari, huduma za matibabu pamoja na kuokoa watu watakaohitaji msaada wa dharura," amesema.