Watatu kizimbani madai ya kusafirisha dawa za kulevya

Watatu kizimbani madai ya kusafirisha dawa za kulevya

Muktasari:

  • Watu watatu wakazi wa Zanzibar wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 10.

  

Dar es salaam. Watu watatu wakazi wa Zanzibar wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 10.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Mohamed Yussuph (35) Mkazi wa Fuoni, Sania Kombo (33) Mkazi wa Fuoni na Nasri Khamis (33) Mkazi wa Mombasa, Zanzibar.

Akiwasomea shtaka linalowakabili leo Jumanne Agosti 24, 2021 Wakili wa Serikali Ashura Mzava amedai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 11, 2021 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA)

Siku hiyo ya tukio, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 10, kinyume cha sheria.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote, kwakuwa Mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kwa kibali maalumu.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka lao, upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo kuomba Mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Luambano baada ya kusikiliza maelezo hayo aliweza kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, 2021 itakapotajwa  

Washtakiwa walirudishwa rumande kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Imeandikwa na Temaluge  Kasuga, Rhoda Kivugo, Robert Nole na Happiness Samson