Watatu waliomwagiana maji ya dripu wasimamishwa kazi

Muktasari:
- Saa chache baada ya video iliyosambaa mtandaoni ikiwaonyesha watumishi watatu wa afya wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa kumwagiana majitiba ya wagonjwa (dripu), yabainika ni wa Hospitali binafsi ya Sakamu na wahusika wamesimaishwa kazi.
Geita. Watumishi watatu wa Hospitali binafsi ya Sakamu iliyopo mkoani Geita wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, kufuatia video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wawili kati yao wakimpongeza mwenzao kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa kutumia majitiba maarufu dripu
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu kuanza uchunguzi wa video hiyo iliyosambaa mtandoni ili kubaini ni kituo cha umma au binafsi.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu leo Jumapili, Desemba 3, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Salvatory Musimu amesema tukio hilo limetokea kwenye hospitali yake na si kwenye Kituo cha Afya Nyankumbu kama ilivyodhaniwa awali.
“Ni kweli tumefuatilia tumeona ni watumishi wetu na ninaandaa taarifa kwa umma kuwajulisha kuwa si Nyankumbu kama ilivyosemakana, ni kwetu na hatua zetu kama taasisi tulizochukua ni kuwaandikia barua ya kuwasimamisha wakati uchunguzi unaendelea,” amesema Dk Musimu.
Siku ya tukio, Dk Musimu kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa muda mfupi baada ya kuzungumza na Mwananchi Digital, amesema tukio hilo lilitokea Ijumaa Desemba 1, 2023.
Mapema Profesa Nagu amesema video hizo hazina uhalisia na eneo linalotajwa (Nyankumbu), hivyo atashirikiana na waganga wakuu wa maeneo husika ili kujiridhisha.
“Nimeiona asubuhi hii tunafuatilia, inaonekana kama hicho kituo kilichoandikwa pengine sicho. Tumeona tu picha za watu, lakini tutafuatilia kuona ni kituo gani, inawezekana pia si jina la kituo kilichoandikwa. Tukishafuatilia tutatoa majibu mpaka tupate ukweli wa tukio lenyewe,” amesema Profesa Nagu.
Katika video hiyo iliyokuwa na maelezo kuwa ni watumishi hao walionekana wanatumia maji ya dripu kwa sherehe yao ya kuzaliwa.
Hata hivyo, maoni ya watu mbalimbali yalijikita kwa Wizara ya Afya kutolea ufafanuzi jambo hilo wakitaka ichukue hatua na kama kuna uvunjifu wa maadili ya utumishi wa afya uwajibikaji uwepo.
Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia ya Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba amesema majitiba yanayotumika kumwekea mgonjwa kupitia mishipa ya damu kikawaida nusu lita huuzwa Sh2, 000 ijapokuwa inategemea na ujazo husika kama ni lita moja ni zaidi ya hapo.