Wateja saba wanusurika gesti ikiteketea kwa moto

Jengo Guest ya West End wakati likiteketea kwa moto.
Muktasari:
- Moto huo unadaiwa kuanza kuwaka leo alfajiri na umeteketeza vitu vingi vilivyokuwa ghorofa ya pili ulikoanzia.
Bukoba. Watu saba waliokuwa wamelala ndani ya nyumba ya kulala wageni ya West End mjini hapa, wamenusurika kifo baada ya moto kuteketeza vyumba vyote sita vya nyumba hiyo iliyopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Julai 20, 2024, Kaimu kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kagera, George Mrutu amesema walipokea taarifa ya moto huo kutoka kwa mwendesha pikipiki saa 10:25 alfajiri.
Amesema kijana huyo ambaye hakujitambulisha jina alifika ofisi za Zimamoto na kuwaeleza kuna jengo la Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba lenye ghorofa mbili jirani na stendi ya zamani ya mji wa Bukoba linaungua moto.
“Tulipofika pale tukakuta ghorofa ya pili ambako ipo hiyo nyumba ya kulala wageni ndiko kunawaka moto na vyumba saba vilikuwa vimeshateketea lakini tulifanikiwa kuudhibiti moto huo usishike majengo mengine,” amesema Kamanda Mrutu.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha wakati moto ulipoanza kuwaka, kulikuwa na wageni watano waliokuwa wamelala hapo na moto huo ulianzia chumba namba 114 ambacho kilikuwa na mgeni.
“Lakini watu wote wamenusurika hawajapata madhara yoyote,” amesema.
Hata hivyo, amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na jeshi hilo linaendelea kuchunguza.

Jengo la Guest ya West End kabla ya kuteketea nyumba ya juu kwa ajali ya moto.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wafanyakazi wa nyumba hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, amedai mgeni aliyelala chumba kilichoanza kuwaka moto alikuwa anavuta sana hivyo anahisi huenda ndiyo chanzo cha moto huo.
"Alikuwa na matumizi makubwa ya sigara kila wakati alikuwa anaagiza tumnunulie sigara sana mara pakiti mbili akimaliza anaagiza moja tena na mara ya mwisho aliagiza paketi tatu,” amedai mfanyakazi huyo.
Shuhuda wa kwanza aliyeuona moto huo aliyejitambulisha kwa jina la Rojazi William, amesema akiwa maeneo karibu na jengo hilo akiwa na wenzake wakitokea kazini alibaini moto ukiwaka juu ghorofani kwa kasi.
“Bahati nzuri lile eneo lina kijiwe cha bodaboda, nao walivyoshtuka wakakimbia kwenda kutoa taarifa kwa mamlaka husika,” amesema William.
Amesema alishuhudia watu waliokuwa ndani ya jengo hilo wakikimbia kushuka chini huku moto ukiwa mkubwa.
William amesema licha ya watu kusaidia kuokoa baadhi ya mali, lakini vitu vingi viliteketea na gari ya zimamoto ilipofika, ilisaidia kuudhibiti moto huo usishike ghorofa ya kwanza kwa kuuzima.
Mwananchi imejitahidi kuwatafuta wamiliki wa jengo hilo kuzungumzia ajali hiyo bila mafanikio.