Watu 11 wakamatwa tuhuma za mauaji ya wanawake nane Mtwara

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemas Katembo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za mauaji ya wanawake nane wa wilayani Masasi mkoani humo katika matukio nane tofauti huku vifo vitano vikisababishwa na wivu wa mapenzi.

Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za mauaji ya wanawake nane wa wilayani Masasi mkoani humo katika matukio nane tofauti huku vifo vitano vikisababishwa na wivu wa mapenzi.

 Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Agosti 11, 2022 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemas Katembo amesema tangu Machi 2022 mpaka leo matukio nane ya mauaji yameripotiwa.

Amesema matukio yote ni wanawake ambao wameuawa na mawili ni ya kuwania mali na matano wivu wa mapenzi na mmoja alimuua ndugu yake kutokana na kuwa na tatizo la akili.

Amesema katika tukio la mauaji ya mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Mwanahawa Hashimu Milanzi (47), Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbaju ambaye alifariki akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Ndanda.

Kaimu kamanda huyo wa Polisi amesema katika uchunguzi uliofanywa na daktari ulibaini kifo chake kimetokana na jeraha kwenye ubongo na kuvuja kwa damu nyingi ambapo mtuhumiwa  Hamza Said Mtila (29) anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi ili kujua sababu ya kutekeleza  mauji hayo ingawa taarifa za awali zinaoonyesha ulikuwa ni wivu wa kimapenzi.

Katika tukio lingine jeshi la Polisi linachunguza kuuawa kwa Fatma  Bakari Suleiman  ambapo majira ya saa 12 kata ya mkuti aligundulika kuuawa na watu wasiojulikana baada ya kulawitiwa kwenye gofu jirani na nyumbani kwao.

Alisema mwili wake ulifanyiwa uchuguzi na kubaini chanzo cha kifo chake ni kukosa hewa baada ya uso kugandamizwa ardhini kwa muda mrefu.

“Kwenye eneo la tukio vilikutwa kitambulisho cha mpiga kura, laini mbili za simu na kofia ambazo zitasaidia kwenye uchunguzi na zitatumika kama vielelezo,” amesema

“Lakini majira ya saa tatu usiku, marehemu akiwa na dada yake waliingia kula chakula cha usiku na haijulikani alitoka saa ngapi ndani hadi asubuhi walipobaini amefariki dunia jirani na nyumbani kwao,” amesema

Kamanda huyo amesema, “watuhumiwa wamekamatwa na wameshafikishwa mahakamani kasoro kesi moja ambayo mtuhumiwa bado hajapatikana.”