Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watu 30, 000 Dar, Mwanza wakutwa na saratani

Meneja wa Mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP), Dk Harrison Chuwa akizungumza wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya uchunguzi wa awali wa magonjw ya saratani katika mradi huo. Ripoti hiyo imebaini watu 30,000 kati ya 800,000 waliofanyiwa uchunguzi wana matatizo ya saratani. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Uchunguzi wa awali uliofanywa na Taasisi ya Agha Khan kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) pamoja na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kuanzia Desemba 2020 hadi Septemba, 2023 umeonesha kati ya watu 800,000 waliofanyiwa uchunguzi, watu 30,000 wana saratani.

Mwanza. Watu 30,000 kati ya 800,000 waliofanyiwa uchunguzi wa awali katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza wamekutwa na saratani mbalimbali huku saratani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume zikiongoza.

Takwimu hizo zimepatikana kupitia uchunguzi wa awali uliofanywa na Taasisi ya Agha Khan kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kuanzia Desemba 2020 hadi Septemba, 2023.

Akizungumza Novemba 28, 2023 jijini Mwanza kwenye mdahalo wa kujadili tafiti na matokeo ya saratani katika mikoa hiyo, Meneja wa mradi huo, Dk Harrison Chuwa amesema uchunguzi huo umefanyika kupitia Mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) wenye thamani ya Sh39 bilioni.

Dk Chuwa amesema watoa huduma 300 katika vituo 50 vya afya mkoani Mwanza na wananchi zaidi ya 5,000,000 wamefikiwa na kujengewa uwezo wa namna rahisi ya utambuzi wa dalili za awali za saratani.

"Mradi wetu unalenga kuhakikisha asilimia 50 ya wagonjwa wanaibuliwa wakiwa katika hatua ya kwanza na ya pili, wakati tunaanzia tumekuta ni asilimia 15 tu ya wagonjwa walikuwa wanakutwa wakiwa katika hatua ya awali huku asilimia 85 wakiwa hatua ya mwisho," amesema Dk Chuwa

Amedokeza kuwa baada ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, kufikia Septemba mwaka huu, idadi ya wagonjwa wanaobainika katika hatua ya kwanza na pili imeongezeka hadi kufikia asilimia 30 huku lengo likiwa kufika asilimia 45 ifikapo Desemba 31, 2023.

Katika hatua nyingine, Dk Chuwa amesema licha ya kusimika mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti (Mammogram) hospitalini hapo (Bugando), bado kasi ya uchunguzi wa saratani hiyo hairidhishi kwani kwa siku inachunguza mtu mmoja ikilinganishwa na uwezo wake wa watu 25 kwa siku.

"Tangu 2022, ni watu 500 pekee ambao wamefika na kuchunguzwa sawa na mtu mmoja kwa siku wakati mashine hiyo inaweza kuhudumia watu 25 kwa siku. Bado Bugando haijaitendea haki hii mashine tunatarajia kuona namba ukiongezeka," amesema 

 Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Saratani Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Nestory Msalu ametaja mwitikio mdogo wa wananchi kupima saratani ya matiti kuchangia idadi ndogo ya watu waliopimwa katika mashine hiyo.

Dk Masalu amesema Bugando inahudumia wagonjwa wapya wa saratani 1,500 kwa mwaka huku watoto wakiwa 200 hadi 300 sawa na asilimia 20 huku asilimia 55 ya wanawake wenye saratani ya shingo ya kizazi na matiti wakifika kwa kuchelewa hospitalini hapo jambo ambalo linaweka ugumu kutibika.

"Kutokana na mwitikio mdogo wa watu kupima tunafikiria kuiweka sehemu inayotakiwa na kuelimisha watu waje wapime. Bugando tulianza kwa kuwapima manesi wetu lakini ni 90 tu walijitokeza kwa hiyo mapokezi ya watu yako chini," amesema Dk Masalu

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa amewataka kujenga utamaduni wa kuchunguza magonjwa ikiwemo saratani ili kuwahi mapema kabla ugonjwa haujafika katika hatua mbaya kutibika.

Mashujaa wafunguka

Shujaa wa saratani ya tezi dume, Deocles Rutatina amesema pamoja na kuugua saratani kwa miaka sita, elimu aliyopewa kupitia mradi huo imemsaidia kuchangamkia matibabu na sasa afya yake imeimarika.

"Tumefanikiwa kuanzisha taasisi yetu ya mashujaa wa Saratani inayoitwa Upendo Cancer Foundation tayari tupo watu 50 Kanda ya Ziwa, lengo ni kutoa elimu, kuibua wagonjwa wapya, kuhamasisha kupata matibabu sahihi, kuwezesha matibabu na kuhamasisha upatikanaji wa dawa zinazohitajika kwa wagonjwa wa kansa," amesema Rutatina

Naye, Jeredina Nzongela amesema wagonjwa wengi wa saratani hukutwa hatua ya tatu na nne ambazo ni ngumu kutibika kwa sababu wanaanzia katika miti shamba huku wengine wakiamini katika mila potofu ikiwemo kuamini kwamba wamerogwa.

"Saratani ni ugonjwa ambao upo na unatibika wala siyo ugonjwa wa kurogwa, hivyo basi kwa uzoefu wangu wa kuugua ugonjwa wa saratani ya tezi dume, njia pekee ya kupona ni kubainika mapema na kuanza matibabu," amesema Nzongela