Watu wanne wauawa kwa risasi Meru

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Arusha, Charles Mkumbo akizungumza na gazeti hili leo kwa njia ya simu alithibitisha mauaji hayo na kuwa kuna watu wengine watano wamejeruhiwa katika tukio hilo.

Watu wanne wameuawa kwa kupigwa risasi na wanaodaiwa kuwa ni walinzi wa msitu wa Mount Meru Kata ya Oldonyosambu.

Kamanda wa Polisi Arusha, Charles Mkumbo akizungumza na gazeti hili leo kwa njia ya simu alithibitisha mauaji hayo na kuwa kuna watu wengine watano wamejeruhiwa katika tukio hilo.

"Tunachunguza ili kujua nguvu iliyotumika kama ilistahili, taarifa za awali tulizonazo ni kwamba wananchi waliingiza mifugo kwenye hifadhi kwa ya ajili ya malisho wakidai kuwa kutokana na ukame, walinzi hao nao walianda operesheni ya kuwakamata wafugaji na mifugo ili wachukuliwe hatua za sheria," alisema.

Alisema awali walinzi hao walifanikiwa kukamata ng'ombe 45 na kuwapeleka kwenye zizi lao maalum lililopo ndani ya hifadhi hiyo, kisha kuendelea na operesheni yao na kukamata ng'ombe wengine 80.

"Wakiwa njiani kuwapeleka kwenye zizi ndipo waliibuka vijana wa kimasaii  wanaodaiwa kuwa na silaha za jadi kisha wakaanza kupambana nao ndipo walinzi wakawashambulia kwa risasi na kusababisha vifo vya watu hao wanne papo hapo huku wengine watano walijeruhiwa, walipelekwa hospitali ya Mount Meru ambapo wamelazwa wakipatiwa matibabu," alisema Kamanda Mkumbo.