Watu zaidi ya 53,000 wachanjwa chanjo ya Uviko-19 Mara

Muktasari:

  • Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Juma Mfanga amesema zaidi ya watu 53,000 wameshapata chanjo ya Uviko-19 mpaka kufikia Novemba 25, 2021 mkoani humo.

Musoma. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Juma Mfanga amesema zaidi ya watu 53,000 wameshapata chanjo ya Uviko-19 mpaka kufikia Novemba 25, 2021 mkoani humo.

Dk Mfanga amesema hayo leo Alhamisi wakati akitoa taarifa ya idara ya afya kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC).

Dk Mfanga amesema kuwa katika awamu ya kwanza mkoa huo ulipokea dozi 25,000 za chanjo ya Johnson Johnson ambazo zilitumika na kuisha na hivyo kulazimika kuomba dozi nyingine 9,850 ya chanjo hiyo katika mkoa wa Mwanza ambazo pia ziliisha Oktoba, 2021.

Amesema kuwa mkoa huo pia ulipokea jumla ya dozi 45,969 ya chanjo ya Sino pharm na kwamba shughuli ya kutoa chanjo kwa wakazi wa mkoa huo zinaendelea katika vituo 285 kutoka vituo 22 vilivyotengwa awali.

" Tuliamua kuongeza vituo vya kutolea chanjo ili kuongeza idadi ya wateja na pia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwani mpango wa chanjo ulilenga kufanya uhamasishaji zaidi kwa jamii ili wapate uelewa wa chanjo na kufanya maamuzi ya kuchanjwa" amesema

Amesema kuwa kabla ya kuanza kutoa chanjo, idara ya afya ilipanga mikakati mbalimbali ili kufanikisha suala hilo ambapo mikakati hiyo ni pamoja na uhamasishaji uliofanywa katika maeneo mbalimbali ikiwemo makanisani, misikitini, misibani, sokoni, visiwani na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.

Amesema kuwa kutokana na uhamasishaji uliofanywa na idara ya afya uelewa kuhusu chanjo ya kuzuia Uviko 19 umeongezeka katika jamii ingawa bado wapo baadhi ya watu wana uelewa mdogo juu ya umuhimu wa chanjo hiyo.