Wauguzi Kahama mikononi mwa Baraza la Kitaaluma

Baadhi ya viongozi na wanachama wa UWT Wilaya ya Shinyanga wakimsikiliza Mganga Mkuu Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndungile (hayuko pichani) alipokuwa akijibu baadhi ya hoja wakati wa mkutano wa jumuiya hiyo ya CCM. Pica na Suzy Butondo
Muktasari:
Wauguzi wanane wanaofanya kazi katika vituo vya huduma ya afya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wamefikishwa mbele ya Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA) kutokana na malalamiko kutoka kwa wagonjwa.
Shinyanga. Wauguzi wanane wanaofanya kazi katika vituo vya huduma ya afya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wamefikishwa mbele ya Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA) kutokana na malalamiko kutoka kwa wagonjwa.
Akizungumza leo Mei 9, 2023 wakati wa kikao kazi cha mafunzo cha wanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Shinyanga, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndungile amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya uongozi kupokea taarifa kutoka kwa wagonjwa wanaolalamikia huduma isiyoridhisha kutoka kwa wauguzi hao.
Mbele ya wajumbe wa mkutano huo ambao pia unahudhuriwa na Makatibu wa CCM kutoka kata za Wilaya ya Shinya, Ndungile amesema mashauri ya wauguzi hao yanaendelea na yako katika hatua mbalimbali mbele ya baraza hilo a kitaaluma.
"Nawaomba wananchi wanapokumbana na tatizo lolote linalohusiana na lugha au kauli zisizofaa, huduma duni au isiyoridhisha katika maeneo ya huduma za afya kuwasilisha malalamiko yao kwa uongozi ili hatua stahiki zichukuliwe zikiwemo za kinidhamu na kitaaluma,’’ amesema Dk Ndungile.
Amewaomba viongozi kuanzia Serikali za Vijiji na Mitaa kuwashirikisha waganga wakuu wa wilaya na waganga wafawidhi wa vituo vya huduma vilivyopo katika maeneo yao kwenye vikao kazi kuwawezesha kupokea na kutatua kero na changamoto za wananchi.
‘’Mnapokuwa na vikao vya vijiji, kata na wilaya muwe mnawaita waganga wakuu na wafawidhi wa wilaya na vituo vyote vya huduma ili wasikilize, kujibu na kutatua kero za wananchi ikiwemo huduma na kauli zisizoridhisha kutoka kwa watoa huduma,’’ amesema Dk Ndungile
Katibu wa UWT Wilaya ya Shinyanga, Lucy Enock amemshukuru Dk Ndungile kwa utayari wa kuhudhuria mkutano huo na uwazi katika kujibu hoja na changamoto zilizowasilishwa na wajumbe huku akiahidi kuwa jumuiya itaendelea kuwashirikisha viongozi wa taasisi za umma katika mikutano yake kwa lengo la kuwawezesha kusikiliza, kupokea na kufanyia kazi hoja na maoni ya wananchi.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga, Rehema Nhamanilo amewataka viongozi na watendaji wengine wa taasisi na ofisi za umma kuiga tabia ya uwazi na uwajibikaji unaoonyeshwa na viongozi wa sekta ya afya huku akimwagia sifa Dk Ndungile kwa kuchukua hatua za kinidhamu na kitaaluma dhidi ya watoa huduma wanaokiuka maadili.
Mbunge wa Shinyanga mjini, Patrobas Katambi ambaye pia anahudhuria mkutano huo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali kadri fedha zinazvyopatikana, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za uhakika za afya.
‘’Hadi sasa, tayari Serikali imetoa zaidi ya Sh1.4 bilioni kuboresha sekta ya afya wilayani Shinyanga ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, zahanati, vituo vya afya na kununua dawa na vifaa tiba,’’ amesema Katambi