Wauza vitabu wadai wasomaji wameongezeka

Muktasari:

  • Mwandishi na wauza vitabu wanasema idadi ya wanaosoma vitabu imeongezeka, likiwemo kundi la vijana.

Dodoma. Ari ya usomaji wa vitabu kwa Watanzania imetajwa kuongezeka ukilinganisha na miaka michache iliyopita licha ya uwepo wa idadi ndogo ya waandishi wa vitabu.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Desemba 2, 2023 na mwandishi wa vitabu, Mchungaji Raphael Lyela wakati akizungumzia uzinduzi wa kitabu cha Hekima za Balozi.

Kitabu hicho ni cha saba katika mfululizo wa vitabu vya Mchungaji Lyela na kwa mwaka huu 2023 hicho kinakuwa kitabu cha pili kitakachozinduliwa na Mkuu wa mkoa.

Mchungaji Lyela amesema tofauti na miaka mitano iliyopo, hivi sasa wananchi wengi wanaonekana kuwa na vitabu karibu maeneo mengi ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri.

Mwandishi huyo ameeleza mwamko huo kwamba umetokana na hamasa kubwa waliyotoa viongozi ikiwemo wale waliotunga vitabu vyao ikiwemo Elimu kupitia vyombo vya habari.

"Tumepiga hatua ukilinganisha na miaka mitano nyuma, vijana wengi siku hizi wanaotembea na vijitabu lakini hata majumbani mwao ukienda unaona vitabu, tuongeze juhudi za kuhamasisha ili twende mbele zaidi," amesema Lyela.

Kuhusu kitabu cha Hekima za Balozi, amesema ni kitabu kilichojaa maarifa na utajiri wa nukuu kutoka kwa watu mbalimbali maarufu Duniani lengo ni kumwezesha msomaji kutambua mwelekeo wa ulimwengu wa sasa.

Alisema mjumuiko wa yaliyomo ndani ya kitabu hicho ni maarifa makubwa ambayo Mkuu wa mkoa atayasema siku ya uzinduzi unaotarajia kuhudhuriwa na viongozi wa mkoa na Kitaifa.

Mwalimu Lilian Godfrey amesema hamasa imekuwa ni kubwa kwenye uandishi na usomaji wa vitabu sehemu kubwa kundi la vijana ndilo lililohamasika zaidi.

Mwalimu Lilian amesema miaka michache nyuma ilikuwa ni ngumu kumuona kijana amebeba kitabu au hata kupita maduka ya vitabu labla kuwe na lazima ya kufanya hivyo hasa wanafunzi wa sekondari na vyuo.

"Sasa hivi kweli tunaona kuna mabadiriko kidogo, we pita kwenye maduka walau unaona watu wamesimama wakiuliza bei za vitabu, lakini hamasa zaidi inatakiwa ili isiwe lazima badala yake uwe utamaduni," amesema Lilian.

Mfanyabiashara wa vitabu katika duka la Capital Bookstore, Christian Elias amesme amesema biashara ya viatu kwa sasa inalipa kwani wengi wamehamasika kununua ukilinganisha na kabla.

Elias amesema vitabu vinavyonunuliwa zaidi ni vya waandishi binafsi na vilivyoandikwa na viongozi wakubwa.