Wavujajasho wanolewa kuikabili mifumo kandamizi ya kibepari

Muktasari:
- Wajasiriamali hao (wavuja jasho) wamepatiwa mafunzo hayo kupitia Shule ya Ushirika Winnie Mandela ikliyoandaliwa na Ushirika wa Wanawake Wavujajasho Manzese (Uwawama) kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kumiliki rasilimali kiushirika.
Dar es Salaam. Wakati mfumo kandamizi wa ubepari ukisababisha ugumu wa maisha hasa kwa wasio na ajira, wajasiriamali wadogo wamepatiwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mifumo hiyo kupitia vyama vya ushirika.
Wajasiriamali hao (wavuja jasho) wamepatiwa mafunzo hayo kupitia Shule ya Ushirika Winnie Mandela ikliyoandaliwa na Ushirika wa Wanawake Wavujajasho Manzese (Uwawama) kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kumiliki rasilimali kiushirika.
Akizungumzia mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Uwawama, Tina Mfanga amesema lengo la mafunzo hayo ya Shule ya Ushirika Winnie Mandela ni kupanda mbegu ya ushirika na umiliki wa pamoja ili kuchochea ari ya ujenzi wa vyombo vya wavujajasho.
Pia, amesema wanalenga kuimarisha mshikamano wa vyama vya ushirika vya wavujajasho ili kuwa na nguvu ya pamoja ya kudai mabadiliko ya kisera na kisheria yatakayochochea ustawi wa vyama vya ushirika vya wavujajasho.
“Shule hii inawapatia wavujajasho jukwaa la kuchochea ufahamu wa pamoja wa kitabaka juu ya umuhimu wa mifumo ya kumiliki rasilimali kiushirika. Mbali na uelewa huo wa kitabaka, shule hii inakusudia kuwawezesha kujengeana uwezo wa kuanzisha vyombo vya mapambano,” amesema Tina.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Sabatho Nyamsenda ameeleza namna ubepari unavyogusa maisha ya kila siku ya wanajamii na kwamba moja ya misingi ya ubepari ni ubidhaishaji ambapo kila kitu kinafanywa bidhaa.
“Zamani ilikuwa mtu akipata kiu, anaweza kuomba maji ya kunywa kwa jirani na akapewa, lakini siku hizi maji ni bidhaa, ukitaka maji ya kunywa unakwenda dukani kununua, hii ndiyo mifumo ya kibepari, inafanya kila kitu kuwa bidhaa,” amesema.
Wakizungumzia magunzo hayo, baadhi ya washiriki wameeleza namna yatakavyowawezesha kuimarisha umoja katika vyama vyao ili kuwa na sauti katika kupigania haki zao za msingi katika shughuli zao.
Katibu wa Ushirika wa Wafanyabiashara wa Ilala, Lucy Marwa amesema amejifunza umuhimu wa ushirika katika kuwafanya wavujajasho kuwa na kauli moja hasa wanapopigania maslahi yao yanayokandamizwa na mifumo ya kinyonyaji iliyoletwa na ubepari.
“Tumejengewa uwezo wa kusimama popote kutetea haki zetu. Tumewasikia wenzetu wanaotoka mikoani wakieleza changamoto ya bei za mazao, kwamba Serikali imekuwa ikiwalipa wakulima bei ndogo. Hayo ndiyo mambo ambayo kupitia ushirika, tunaweza kupigania,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Pwani, Ngobele Msamau amesema kupitia mafunzo hayo amejifunza namna changamoto ya ardhi imekuwa ikisababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji na kwamba anayesababisha hilo ni serikali za vijiji.
“Nimetambua kwamba umoja ni nguvu katika kutetea maslahi yetu. Tungepata elimu hii mapema, tungeweza kuzuia hii migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa sababu tunakuwa tunajua anayesababisha ni nani,” amesema.
Katika mafunzo hayo, pia, walikuwepo washiriki kutoka Afrika Kusini ambao walikuja kujifunza na kubadilishana uzoefu na wavujajasho wa Tanzania na kujifunza namna wanavyokabiliana na mifumo ya kibepari.
“Mazingira ya ushirika ya Tanzania yanafanana na yale ya Afrika Kusini kwa kiasi Fulani, tofauti ni kwamba sehemu kubwa ya ardhi ya Afrika Kusini inamilikiwa na wazungu wachache, tulipopata uhuru, ardhi haikurudishwa kwa watu weusi, hivyo walibaki kuwa vibarua migodini,” amesema Janine Lange, mwelimishaji kutoka Kituo cha Maendeleo cha Tshisimani cha huko Afrika Kusini.
Lange amesema vyama vya ushirika vya Afrika Kusini vinapata ruzuku kutoka serikalini na kwamba ushirika umekuwa ukizalisha kwa wingi. Amesema asilimia 75 ya vyakula nchini Afrika Kusini vinazalishwa na ushirika.