Wazazi wagomea michango ya chakula shuleni
Picha na Oxfam
Muktasari:
Hayo yalisemwa jana na wajumbe wa kamati za shule za msingi wilayani humo mbele ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Waziri Moris walipokuwa wakifunga mafunzo ya kupanga, kusimamia na kutekeleza majukumu ya maendeleo ya shule kwa lengo la kuongeza ufaulu.
Arusha. Wazazi wa wanafunzi wa shule 87 za Wilaya ya Karatu wamegoma kutoa michango ya chakula shuleni wakidai ni miongoni mwa huduma zinazotolewa bure na Serikali.
Hayo yalisemwa jana na wajumbe wa kamati za shule za msingi wilayani humo mbele ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Waziri Moris walipokuwa wakifunga mafunzo ya kupanga, kusimamia na kutekeleza majukumu ya maendeleo ya shule kwa lengo la kuongeza ufaulu.
Walisema wenzao wa shule 18 ndiyo wanaopata chakula baada ya wazazi na walezi kukubali kuchangia.
Wanakamati hao walisema wazazi wamekuwa wakiitafsiri vibaya sera ya elimu bure kwa kukaidi maazimio ya vikao vya kuchangia chakula cha wanafunzi wao wanapokuwa shuleni na michango ya ukarabati wa samani.
Mwenyekiti wa Shule ya Ako, Judith Kimaro alisema suala hilo ni sawa na kuihujumu Serikali ambayo inatoa elimu bure, lakini kiwango cha ufaulu hakipandi kutokana na watoto kukosa chakula shuleni.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, alisema Serikali iliposema elimu bure haikumaanisha kuwa ni pamoja na sare za wanafunzi wala chakula shuleni, bali gharama za utoaji elimu.
Ofisa Elimu ya Msingi wilayani Mbulu, Papakinyi Kaai alisema wanataka kupandisha kiwango cha ufaulu kifikie asilimia 80 kutoka 60.