Wazazi walalamikia michango ya rimu ya makaratasi shuleni

Rimu ya makaratasi yakiwa yamepangwa.
Muktasari:
Rimu moja ya karatasi inauzwa kwa bei kati ya Sh15, 000 hadi Sh20, 000 kulingana na ubora, jina la biashara na umbali wa eneo kutoka ama miji mikuu au vituo vya kibiashara nchini.
Shinyanga. Wazazi wa wanafunzi wa shule za sekondari Manispaa ya Shinyanga wamelalamikia sharti la kila mwanafunzi kutakiwa kuepeleka shuleni rimu moja ya makaratasi kila mwaka kwa madai ya kutumika kuchapia mitihani ya majaribio.
Wakizungumza na Mwananchi leo Mei 4, baadhi ya wazazi walisema mchango wa makaratasi hayo imekuwa kero kama ilivyokuwa wakati wa michango ya Sh500 hadi Sh1, 000 ya mitihani ya ajaribio ya kila mwisho wa wiki.
"Wazazi tunapata shida sana, hasa wale wenye watoto zaidi ya mmoja anayelazimika kutumia kati ya Sh17, 000 hadi Sh20, 000 kwa kila mtoto. Usipolipa hiyo fedha mtoto anagoma hata kwenda shule kwa kuogopa adhabu ya viboko,” anasema Juliana Mwandu mkazi wa Ngokolo.
Mazazi mwingine, Aisha Mohamed, mkazi wa mtaa wa Stendi Manispaa ya Shinyanga amesema wakati mwingine wazazi na walezi hulazimika kukopa kutoka maduka ya vifaa vya shule kuwezesha watoto wao kupata rimu ya makaratasi za kupeleka shuleni.
‘’Kuna wakati tunalazimika kutumia fedha ya chakula kuwanunulia watoto rimu; usimnunua rimu mtoto ananyong’onyea huku akigoma kwenda shule. Ukimlazimisha anaenda huku akiwa Analia,’’ anasema Aisha
Akizungumzia madai hayo, Msitahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi kuhusu uongozi wa baadhi ya shule za sekondari kuwachangisha fedha au kuwataka kupeleka rimu za makaratasi kwa ajili ya mitihani ya majaribio.
‘’Wakati wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule za sekondari wanadai kutakiwa kuchangia rimu ya makaratasi, wenzao wenye watoto shule za msingi wao wanadai kuchangishwa Sh500 kila wiki kwa ajili ya mitihani ya majaribio kila wiki,’’ amesema Masumbuko
Meya huyo amedai kupokea taarifa za baadhi ya walimu kuwaadhibu wanafunzi wasiotoa michango hiyo.
‘’Kutokana na madai hayo, tayari uongozi wa Manispaa umewaagiza watendaji wa kata zote kufuatilia taarifa hizo kubaini ukweli ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika wanaokiuka maelekezo ya Serikali ya kupiga marufuku michango yote,’’ amesema Meya Masumbuko
Amesema kwa hesabu za kawaida, shule yenye wanafunzi 200 hukusanya rimu za makaratasi 200 huku skihoji uhalisia wa matumizi ya karatasi hizo.
"Rimu moja ina karatasi 500; kwa hesabu ya kawaida ni kwamba rimu 200 zina makaratasi 100, 000. Sasa tujiulize hiyo mitihani inachapwa kwa idadi ya karatasi kwa mwaka. Hapa kuna tatizo ambalo lazima tulitafutie ufumbuzi,’’ amesema Masumbuko akielekeza Idara ya elimu kufuatilia madai hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, John Tesha ameahidi kufuatilia suala hilo kubaini matumizi ya makaratasi yote yanayokusanywa kutoka kwa wazazi.