Waziri Mkuu amshukuru Rais Samia kubaki ndani ya Serikali

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya mawaziri wengine kwa kuendelea kuwaamini wabaki ndani ya Serikali.

 Ameyasema hayo katika hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali walioteuliwa jana iliyofanyika jijini Dodoma leo.

Majaliwa amesema watumishi walioapa leo Jumatatu wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa weredi na uadilifu wa hali ya juu.

"Kuwapo kwao hapa tunaamini wanakuja kuimarisha utendaji ndani ya Serikali, Spika ameeleza mengi na mimi kwa niaba ya watendaji wote ndani ya serikali tukuhakikishie kuwa tutawajibika kikamilifu kutekeleza maelekeo yako. Tunatambua maelekezo yako pia ni ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Watanzania wana imani na Serikali yako.

Amesema maelekezo yake watayatekeleza kwa nguvu zote, uaminifu na uadilifu mkubwa.

Amesema kwa nafasi yake anayofursa ya kukutana na mawaziri, manaibu waziri, makatibu na manaibu katibu wakuu kupitia vikao vya kitendaji, hivyo mengi watahabarishana huko.