Waziri Mkuu: Wakurugenzi pelekeni watumishi vijijini
Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza wakurugenzi kupitia ikama ya watumishi ili maeneo walikozidi wapunguzwe kupelekwa maeneo mengine.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni leo Juni Mosi, 2023 wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Mtera (CCM), Livingston Lusinde.
Katika swali lake kwa Waziri Mkuu, Lusinde amehoji ni lini Serikali itapeleka wataalamu wa afya ambao wataendana na vifaa vya kisasa vilivyopelekwa katika vituo vya afya vilivyojengwa nchi nzima ikiwemo Jimbo la Mvumi.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amekiri kuwa Serikali imekamilisha hatua ya kwanza ya ujenzi wa vituo vya afya na hatua ya pili ya upelekaji wa vifaa sasa inafuata kupeleka wataalamu.
Amesema wakati mchakato wa ajira ukiendelea, lakini uko mpango wa kuwaongezea ujuzi wataalamu wa afya kupitia warsha, semina na makongamano.
“Lakini nitoe agizo hapa kwa wakurugenzi wa halmashauri kupitia ikama ya watumishi wao ili walipozidi waweze kupunguzwa na hasa maeneo ya mijini, lazima tuwapeleke vijijini kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” amesema Majaliwa.
Amesema serikali ya awamu ya tano na sita imefanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu katika vituo vya afya nchini.
Hata hivyo Waziri Mkuu amekiri kuwa, kuna mahitaji ya watumishi wengi kwa sasa na kwamba ajira zinaendelea kutolewa kulingana na vibali.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezungumzia utekelezaji wa miradi ya Mtwara korido kuwa unakwenda vizuri ikiwemo maboresho ya barabara na bandari.
Ameeleza hayo kutokana na swali lililoulizwa na Dk Teya Ntala ambaye amehoji mkakati wa Serikali kuhusu Mtwara korido.
Waziri Mkuu amesema mradi huo umeasisiwa na Serikali na akakiri kuwa na yeye ni mdau katika suala hilo hivyo akasema litasimamiwa kikamilifu.