Waziri Tax aieleza Jeshi lilivyoimarisha ulinzi miaka 60 Muungano

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax

Muktasari:

 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema moja ya mafanikio yaliyofikiwa na wizara hiyo kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,  ni wizara hiyo kuongozwa na waziri mwanamke ambaye ni yeye.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema jukumu kubwa la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni ulinzi na usalama wa raia wake jukumu ambalo wamelitekeleza kwa kipindi cha miaka yote 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika Aprili 26, 1964 chini ya waaasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Leo Jumatano April 3, 2024, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amezungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya wizara hiyo kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema dira na dhima ya kuundwa kwa wizara hiyo ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchini unakuwa imara na ndicho kinachoendelea, kwani Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liko imara kila siku na litaendelea kuwa imara.

Amesema mchango mwingine mkubwa wa JWTZ katika miaka 60 ya Muungano, ni ulinzi madhubuti wa mipaka yetu, Uhuru, na Katiba nchi imeendelea kuwa imara na yenye amani katika awamu zote.

“Wakati Watanzania wanalala usiku na mali zao zinakuwa salama wakumbuke kuwa kuna watu ambao hawalali wanakesha wakilinda mipaka ya nchi yetu, kuhakikisha usalama uhuru na Muungano wetu unakuwa salama,” amesema Dk Tax.

Aidha, amesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali ya ukakamavu, uzalendo na uzalishaji mali kupitia mafunzo yanayotolewa na jeshi la kujenga Taifa ambapo mpaka sasa limetoa ajira 36,479 kupitia miradi mbalimbali ya uzalishaji mali inayosimamiwa na jeshi hilo.

Amesema moja ya mafanikio makubwa ambayo wizara hiyo imeyapata ni kuwa na waziri mwanamke kati ya mawaziri 17 ambao wameiongoza wizara hiyo tangu uhuru na kuondoa kasumba iliyojengeka kuwa wizara hiyo ni lazima iongozwe na wanaume tu.

“Na Waziri huyo ni mimi hapa ambaye mwaka 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliniteua kushika wadhifa huu na bado ameendelea kuniamini, hivyo katika ya mafanikio makubwa na hili ni mojawapo ameondoa kasumba tuliyokuwa nayo kuwa ni wanaume pekee ndiyo wanaoweza kuongoza Wizara hii,” amesema Tax.

Amesema mafanikio mengine ambayo yamefanywa na wizara hiyo ni kushiriki kwenye matukio ya uokozi wa watu na mali zao hasa pale Taifa linapokumbwa na maafa kama ajali, mafuriko na majanga mengine ambapo jeshi la wananchi wa Tanzania limekuwa mstari wa mbele kutoa msaada.

Tax amesema ili kuliimarisha Jeshi, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa Wanajeshi na Watumishi wa Umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu, kwa kuwapatia makazi bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali, kupandisha vyeo kulingana na sifa, vigezo na taratibu.

Amesema hadi sasa Serikali imekwishajenga  nyumba za makazi katika kambi mbalimbali za jeshi kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Mwanza, Pemba, Pwani, Rukwa, Tabora, na Tanga ujenzi ambao kwa kiasi kikubwa umepunguza uhaba wa nyumba pamoja na changamoto zitokanazo na wanajeshi kuishi uraiani.

Kwa upande wa kimataifa na kikanda, Dk Tax amesema Serikali imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuhakikisha hali ya Ulinzi na Usalama inaimarika.

Kwa sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ inashiriki katika operesheni mbalimbali za Umoja wa mataifa kwa kutoa vikosi vya kulinda amani katika nchi za DRC, Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na Lebanon.

Amesema na pia JWTZ inashiriki katika operesheni za kuleta amani nchini Msumbiji kupitia Misheni ya SADC (SADC Mission in Mozambique - SAMIM) iliyopo chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Misheni ya kuleta Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC) iliyopo chini ya SADC.

“Aidha, JWTZ limeendelea kutoa maafisa wanadhimu wakuu katika misheni za Umoja wa Mataifa na misheni za kikanda,” amesema.