Waziri Tax: Wanawake ni sehemu muhimu katika ulinzi na usalama

Baadhi ya wahitimu wa Stashahada na Shahada ya Uzamili ya mafunzo ya ulinzi na usalama katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti, wilayani Arumeru wakiwa katika mahafali yao leo Jumamosi Juni 15, 2024.
Muktasari:
- Mahafali ya tatu na ya 39, yamefanyika katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti wilayani Arumeru
Arusha. Serikali imesema wanawake ni sehemu muhimu ya ulinzi na usalama jeshini na kwamba wakipewa nafasi wana uwezo wa kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema hayo leo Juni 15, 2024 wakati akitunuku stashahada na shahada ya uzamili ya mafunzo ya ulinzi na usalama kwa maofisa 69.
Mahafali hayo ya tatu na ya 39, yamefanyika katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti wilayani Arumeru.
Amesema idadi ya wanawake katika jeshi hasa katika kozi kama za ulinzi na usalama, inapaswa kuzingatiwa na kuwa moja ya kielelezo cha uwezo wa wanawake katika uongozi ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Kutokana na sababu hiyo, amewataka wanawake walioko jeshini kuonyesha uwezo na utendaji kazi pale wanapopewa nafasi.
“Ni wazi waliofanya vizuri leo ni wanaume, hivyo naamini katika awamu ijayo katika masomo ya ulinzi na usalama hali itakuwa tofauti na nihimize zaidi wanawake mnapopewa nafasi, onyesha uwezo wako vizuri,” amesema Waziri huyo.
Kutokana na kuongezeka kwa changamoto za ulinzi na usalama katika ngazi za kikanda na kimataifa, Dk Tax aliwataka wahitimu hao kutoka nchi 16 za Bara la Afrika kujitahidi kutatua changamoto hizo.
Waziri huyo amewataka wahitimu hao kutumia mafunzo hayo kuhusu ulinzi na usalama waliyoyapata kuwafanya kuwa viongozi wazuri wa vikosi vya ulinzi katika nchi zao.
Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti, Brigedia Jenerali Stephen Mnkande amesema wahitimu 69 wamejengewa ujuzi wa kutambua na kuelewa ili kufanya uamuzi sahihi katika masuala ya ulinzi na usalama.
Amesema elimu waliyoyapata katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Duluti ina ubora na viwango vya juu itakayowasaidia katika kufanya uamuzi sahihi nyakati za amani au vita.
“Mtapimwa na nchi zenu nyakati za amani na vita, muwe tayari kutumia elimu mliyoipata hapa,” amesema Brigedia Jenerali Mnkande.
Wahitimu hao wa kozi ya ulinzi na usalama wanatoka nchi 16 zikiwamo Tanzania, Eswatini, Botswana, Ethiopia, DR Congo, Burundi, Misri na Kenya.
Nchi nyingine ni Msumbiji, Malawi, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Zimbabwe, Zambia na Uganda.