Waziri Ummy atoa matumaini bima ya afya kwa wote

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hamasa na elimu ya kutosha ikitolewa kwa wananchi kujiunga kwenye bima ya afya kwa wote kuna uwezekano wa kupunguzwa kwa viwango vya uchangiaji au kuongezwa mafao ya huduma zaidi.Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hamasa na elimu ya kutosha ikitolewa kwa wananchi kujiunga kwenye bima ya afya kwa wote kuna uwezekano wa kupunguzwa kwa viwango vya uchangiaji au kuongezwa mafao ya huduma zaidi.

Pia amesema, “bima ya afya kwa wote si jambo jepesi, Watanzania wanahitaji huduma za afya bila kuwepo kikwazo cha fedha.”

Pia, amesema hakuna eneo lolote kwenye Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ilikowekwa viwango vya uchangiaji bali Serikali inachosisitiza wanannchi kujiunga na bima ya afya ili kupata huduma bora za afya.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Januari 25, 2023 kupitia mjadala wa Twitter Space ya Mwananchi unaojadili ‘mambo gani muhimu yazingatiwe kwenye bima ya afya kwa Wote.”

Amesema,“muswada huu unaweka misingi ya kumwezesha Mtanzania apate huduma bora za afya atapaswa kujiunga na bima ya afya.”

Waziri huyo amesema, “tumepokea maoni na ushauri wote uliotolewa kwenye jukwaa hili la Mwananchi TwitterSpace. Nimeona watu waliochangia wanakubaliana na umuhimu wa bima ya afya.”

Amesema, hapa tuangalie jinsi ya kuwezesha kila Mtanzania kupata bima ya afya bila kuwepo kikwazo cha fedha, “hakuna sehemu yoyote kwenye muswada tumeweka kiwango cha fedha cha kuchangia, tulichosema ni mwananchi ajiunge na ‘scheme’ yoyote ya bima ya afya.” 

“Kwenye suala la ubora wa huduma tusipokuwa makini wote wenye bima za afya wataenda hospitali binafsi, hilo tuliliona ndio maana tumeboresha huduma kwenye vituo na hospitali za Serikali tumeongeza vifaa tiba, miundombinu na watumishi kilichobaki ni suala la utendaji na uwajibikaji,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishana wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware amesema  mambo yote ya msingi yamezingatiwa kwenye muswada wa bima ya afya ikiwemo vitita vinavyopendekezwa.

Amebainisha bima ya afya itakwenda kuongeza upatikanaji wa huduma na kuongeza ushindani kwenye sekta ya afya.

Naye Rais wa Tanzania Health Summit, Dk Omary Chilo amesema ubora wa huduma za afya lazima ziendane na uchagiaji.

“Sasa hivi wenye bima wanakimbilia hospitali za binafsi kuliko za serikali kwa sababu ya ubora wa huduma,” amesema

Pia amesisitiza kinga ikizingatiwa idadi ya watu wanaohitaji ya watu wanaofuata matibabu hospitali itapungua.

Sheria ya bima ya afya inayopendekezwa itaitambua NHIF kama Mfuko wa Bima ya Afya wa Umma utakaohudumia watumishi wa umma na wananchi wengine watakaochagua kujiunga na mfuko huo.

Endapo Bunge litapitisha Muswada huo katika mkutano wa Bunge unaoanza Januari 31, 2023 kuwa sheria na Rais Samia Suluhu Hassan akausaini kuwa sheria, unatarajiwa kuanza kutumika Julai mosi, 2023.