Shinyanga. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka watendaji na watoa huduma sekta ya afya kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao ikiwemo inayotakaza kutoa siri na taarifa za wagonjwa.
Akizungumza na watumishi wa sekta ya afya mkoani Shinyanga leo Julai 13, 2023, Waziri Ummy ameonya kuwa Serikali itawachukulia hatua za kisheria, kikanuni na kitaaluma watumishi wote watakaotenda kosa la kutoa siri za wagonjwa na makosa mengine ya kitaaluma kitaaluma.
Akiwa kwenye ziara yake ya kukagua utoaji wa huduma za afya mkoani Shinyanga, Waziri huyo mwenye dhamana ya afya ametoa mfano wa taarifa za mwanaume mmoja kudaiwa kujikata uuma kwa kile alichodai ni kukosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa akihisi huenda zimevujishwa na wataalam wa afya waliomhudumia mtu huyo.
"Hapa naangalia kwenye mitandao ya kijamii kuna taarifa ya mwanaume kujikata uume kwa sababu hawezi kushiriki tena tendo la ndoa….nimemuagiza Mganga Mkuu afuatilie kufahamu nani katoa taarifa ya mgonjwa huyo," amesema Mwalimu
Kuhusu huduma, Waziri Ummy amewataka watumishi wa sekta ya afya kupunguza semina na kongamano ili kupata fursa na muda mwingi wa kuwahudumia wagonjwa.
Akizungumzia utoaji wa dawa kwa wagonjwa, Waziri Ummy amewataka mafamansia kuongeza umakini kwa kutoa dawa sahihi na kwa kiwango kulingana na maelekezo ya daktari kulinda afya ya watu.
Waziri Ummy amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuajiri wataalamu wa afya kwa mikataba maalum ya muda kulingana na mahitaji ya halmashauri zao na kutumia fedha za mapato ya ndani kuwalipa watakaoajiri katika mpango huo.
‘’Hii itasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi wa sekta ya afya katika ngazi ya halmashauri wakati Serikali ikiendelea kutekeleza michakato ya ajira kumaliza tatizo hilo,’’ ameagiza Waziri Ummy
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndugile amemweleza Waziri Ummy kiongozi huyo wa wizara kuwa kiwango cha huduma za afya mkoani humo kimeimarika huku upatikanaji wa dawa ukifikia zaidi ya asilimia 89.
‘’Pamoja na mafanikio hayo, bado tunakabiliwa na tatizo la upungufu wa watumishi, hasa madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa,’’ amesema Dk Ndugile
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi amesisitiza nia ya Serikali ya kuendelea kuboresha huduma katika sekta ya afya, huku akiwataka watendaji na watumishi kutimiza wajibu wao wa kuhudumia wananchi katika vituo na maeneo yao ya kazi.