Wezi waiba mashine ya ATM
Muktasari:
Watumia tingatinga waliloliiba jirani na eneo hilo na kuing’oa mashine hiyo ambayo inatumiwa na watu wengi
Antrim. Ireland. Majambazi wameing’oa ukutani na kutokomea na mashine ya kielektroniki ya kutolea pesa (ATM) nchini Ireland ya Kaskazini.
Majambazi hao walitumia tingatinga ambalo pia waliliiba na kuinyofoa ATM hiyo kutoka kwenye ukuta wa duka moja katika kaunti ya Antrim.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, tukio hilo limetokea saa 9:00 usiku wa Jumatatu. Polisi wamethibitisha kuwa jengo hilo limeharibiwa vibaya.
Mmiliki wa duka hilo, Walter Millar amesema ATM hiyo ilikuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo hata wa kutoka nje na kwa sasa hakuna hata dalili ya kupata mashine nyingine.
Alisema wakati anapata taarifa hizo kutoka kwa wananchi alidhani ni uongo kwa sababu juzi ilikuwa ni siku ya wajinga duniani lakini kumbe alikuwa akiambiwa ukweli.
"Ninachoweza kusema ni kuwa, wametumia tingatinga ambalo waliliiba kwenye eneo moja la ujenzi eneo la jirani, wakainyofoa mashine na kuipakia kwenye gari na kuondoka nayo," amesema.
"Tulipokea simu kuhusu tukio hilo saa 3:00 usiku kuwa tingatinga linaungua moto eneo hilo," amesema mkuu wa polisi eneo hilo, Richard Thornton.
Amesema tangu mwanzoni mwaka huu mashine saba za ATM zimeibiwa. Polisi wanaamini kuna makundi kadhaa ya majambazi ambayo yanajihusisha na wizi wa mashine hizo.
Amesema wamiliki wa maduka sasa wanaogopa kuweka mashine hizo kwenye maeneo yao ya biashara na tayari watu kadhaa wametahadharisha endapo wizi huo utaendelea basi watalazimika kuzitoa mashine hizo.