Wivu wa mapenzi mzimu mpya wa vifo vya mauaji Afrika Mashariki
Muktasari:
- Zaidi ya asilimia 35 ya vifo vya wanawake vinavyotokana na mauaji husababishwa na wenza wao, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyochapishwa hivi karibuni inasema.
Dar es Salaam. Zaidi ya asilimia 35 ya vifo vya wanawake vinavyotokana na mauaji husababishwa na wenza wao, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyochapishwa hivi karibuni inasema.
Utafiti huo unaoitwa ‘understanding and addressing violence against women’ unasema ni asilimia saba tu ya vifo vya mauaji ya wanaume husababishwa na wenza.
Hata hivyo, ripoti hiyo inasema huenda idadi ikawa kubwa zaidi kutokana na takwimu katika baadhi ya nchi hasa zinazoendelea kukosekana.
Matokeo ya utafiti huo yanaakisi hadi Afrika Mashariki hasa Tanzania, Kenya na Uganda ambako matukio ya wapenzi kuuana yanaongezeka kila siku.
Mauaji ya mapenzi nchini
Kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, matukio 14 ya wapenzi kuuana kwa wivu wa mapenzi yameripotiwa na vyombo vya habari nchini, wastani wa matukio matano kila mwezi. Takwimu hizo ni kubwa zikilinganishwa na nyuma.
Kati ya matukio yaliyotikisa nchi ni la Julai 26 ambalo Maria Sakware wa mkoani Manyara alifariki wakati akitibiwa baada ya kushambuliwa kwa fimbo na mume wake, Petro Fabiano baada ya kumtuhumu kuchukua Sh10,000 bila ridhaa yake.
Siku mbili baadaye, mwalimu wa Shule ya Sekondari Tanga ya moani Rukwa, Emmanuel Jerome (32) alidaiwa kumnyonga mke wake, Lucy Nshoma (34) katika nyumba ya kulala wageni na yeye kujinyonga kwa kamba siku moja baadaye mkoani Katavi.
Agosti 10, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro lilitangaza kumshikilia Msafiri Nasibu (31) mkazi wa Maskati mjini humo kwa tuhuma za mauaji ya mke wake Mariam Vitaris (19) na mtoto wake wa miaka miwili chanzo kikidaiwa ni mgogoro wa kifamilia.
Septemba 7, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilitangaza kumshikilia Peter Mwakiposile kwa tuhuma za kumuua mkewe Aisha Ramadhani mkazi wa Chidachi kwa kumpiga kwa kosa la kuchelewa kurudi nyumbani akitafuta fedha za kurejesha kwenye kikundi cha kicoba.
Vyombo vya habari viliendelea kuutaarifu umma juu ya matukio mauaji ya wapenzi na karata kuangukia jijini Mbeya ambako Septemba 14 kulikuwa na vifo vinne vya familia moja.
Vifo hivyo vilitokea katika Kijiji cha Kibumbe wilayani Rungwe huku sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi ambapo baba alimuua mke kisha watoto halafu akajiua yeye mwenyewe.
Kenya
Hali si shwari nchini Kenya ambapo wastani wa matukio 30 ya mauaji ndani ya familia yameripotiwa Oktoba.
Julai 16 mwaka jana, vyombo vya habari viliripoti kifo cha Celestine Muthengei (19) mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Mount Kenya aliyedaiwa kuuliwa na mpenzi wake baada ya kujeruhiwa kwenye hosteli za chuo hicho kutokana na wivu wa mapenzi.
Septemba 26, mwanamke mmoja alidaiwa kumuua mume wake halafu akajinyonga akiwaacha watoto watatu bila wazazi katika Kaunti ya Tharaka Nithi kwa wivu wa mapenzi.
Jonathan Shikulu alidaiwa kumpiga mke wake Faith Nanzala (31) hadi kufa baada ya kumzuia kuoa mke wa pili, tukio hilo lilitokea Oktoba 9 mwaka huu nchini humo.
Oktoba 17 polisi katika Kaunti ya Trans-Nzoia walitangaza kumsaka Andrew Mulati kwa tuhuma za kumuua mkewe Joan Makungu (35) kwa kumchoma kisu. Tukio hilo lilidaiwa kutendwa Kijiji cha Koros II.
Uganda
Gazeti la Daily monitor limeripoti zaidi ya matukio 10 za mauaji ya wapenzi ndani ya miezi mitatu.
Polisi wa Kyoga Mashariki walitoa taarifa za kifo cha Abdallah Okalebo (48) na uchunguzi wa awwa polisi ulihusisha wivu wa mapenzi kwamba marehemu alikuwa na mahusiano na mwanamke aliyekuwa na wanaume wengine.
Septemba 24, Jeshi la Polisi nchini humo lilitangaza kufuatilia mauaji ya mke na watoto wawili yanayodaiwa kufanywa na Faisal Muwanguzi (baba wa familia hiyo) ambaye baadaye aliizika miili hiyo nyuma ya nyumba yao iliyopo katika Kijiji cha Bwotansimbi.
Jeshi la polisi wilayani Pader nchini humo, Septemba 22 lilitangaza kumshikilia James Odong (46) wa Kijiji cha Oluk kwa tuhuma za kumpiga mke wake, Hellen Akumu hadi kumuua baada ya kumkuta akiwa na mwanaume mwingine chumbani kwao.
Ripoti za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha asilimia 69 ya wanawake waliuawa mwaka 2017 kwa makusudi na wapenzi wao. Hii inamaanisha zaidi ya theluthi mbili za mauaji ya wanawake hufanywa na wapenzi wao.
Takwimu za mauaji Tanzania
Wakati matukio ya mauaji ya wapenzi yakiongezeka, takwimu za Jeshi la Polisi kwenye ripoti ya ‘Tanzania in Figures 2021’ inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuongezeka kwa mauaji mwaka 2021 kwa asilimia 3.1.
Mauaji yaliyorekodiwa mwaka 2020 yalikuwa 2,225 ambayo yaliongezeka hadi 2,294 mwaka 2021.
“Mwaka 2017 kulikuwa na mauaji 3,026 yaliyoongezeka kutoka 2,619 ya mwaka 2019. Mwaka 2018 kulikuwa na matukio 2,655,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Kutokana na takwimu hizo, wastani wa mauaji 191 yalifanyika kila mwezi nchini na mauaji sita hadi saba yakiripotiwa kila siku mwaka 2021.
Wanasaikolojia wanasemaje
Mwanasaikolojia Neema Mwamkina alisema maumivu aliyoyapitia mtu kwenye mahusiano yake ya awali yanaweza kusababisha kuua au kuchukua uamuzi mgumu kwenye uhusiano mpya endapo atakosewa na mwenziwe.
“Maumivu aliyowahi kupitia yanakuwa moyoni hivyo mtu wa hivi akiingia kwenye mahusiano mapya anakaa chonjo muda wowote ikitokea amekwazwa na mpenziwe anaweza kufanya kitu kibaya,” alisema Neema.
Makuzi na malezi ya mtoto yasipokuwa sahihi, alisema yanaweza kusababisha mtu kuwa katili ukubwani na kufanya vitendo vya ajabu ikiwamo kuua.
“Makuzi na malezi yanachangia haya yote kutokea. Mtu aliyelelewa kwenye mazingira ya kunyanyaswa kwenye familia yake akiwa mkubwa moyo wake utakuwa na maumivu na kisasi muda wote na anaweza kuchukua uamuzi kama kumuua mwenzi wake kwa makosa madogo,” alisema na kuongeza:
“Kuna familia mtoto hajawahi kupendwa tangu utotoni, muda wote anapigwa na kufokewa, huyu akikua lazima na yeye atakuwa na tabia hizo kutokana na hasira alizozihifadhi moyoni.”
Charles Muhando, mwanasaikolojia mwingine alisema sababu kubwa ya matukio hayo ni changamoto ya afya ya akili jambo linalowasababisha kufanya matukio yasiyo ya kawaida.
“Baadhi ya watu wanaishi na changamoto ya afya ya akili bila wao kujua, hii inawasukuma kufanya vitu ambavyo sio sahihi kwa watu wao wa kawaida,” alisema Muhando.
Nini kifanyike
Neema alishauri wapenzi wakipata changamoto wawaone wanasaikolojia watakaowasaidia kuzuia kufanya uamuzi mbaya.
“Kitu muhimu watu wanapoingia kwenye mahusiano ni kupata tiba ya kisaikolojia, wanasaikolojia tupo wengi na tunaweza kumjenga mtu akaachana na mawazo mabaya kwa mpenzi wake,” alisema.
Mhando ameimba Serikali kuweka utaratibu wa kliniki maalumu ya ushauri kwenye maeneo ambayo matukio ya namna hiyo yanatokea kwa wingi.
“Serikali inaweza kuwatumia wataalamu wa afya ya akili kupiga kambi maeneo ambayo matukio kama hayo yanatokea ili kutoa elimu na ushauri,” alisema.